
Wanawake wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), Dar es Salam wametembelea Gereza la Segerea na kutoa misaada mbalimbali kwa wafungwa, ikiwa ni sehemu ya kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yanayoadhimishwa kila mwaka Machi 8.
Ziara hiyo pia imekuwa muendelezo wa maadhimisho ya miaka 25 ya chuo hicho, ambapo taasisi imekuwa ikitekeleza shughuli za kurejesha kwa jamii kupitia matendo ya kijamii na misaada kwa makundi yenye uhitaji.
Akizungumza wakati wa kukabidhi misaada hiyo, Zena Hussein, Meneja wa Sehemu ya Mafunzo kwa Njia ya Mtandao TPSC, aliyemwakilisha Mkuu wa Chuo, amesema wanamshukuru Mkuu wa chuo kwa kuwawezesha kutekeleza jukumu hilo la kijamii, akieleza kuwa lengo ni kuonyesha upendo na mshikamano kwa wafungwa kama sehemu ya jamii.
Amesema kuwa, kama wanawake wafanyakazi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, wameona umuhimu wa kutambua kundi hilo na kujitoa kwa moyo wa huruma wakiamini kuwa si kila aliyepo gerezani ni mkosaji wa kukusudia, bali baadhi yao wamejikuta katika mazingira magumu yasiyotegemewa. Ameongeza kuwa misingi ya dini, kwa Waislamu na Wakristo, inahimiza kusaidia wahitaji na kuwa watoaji, hivyo wameamua kupeleka kile walichoweza kumudu.
Miongoni mwa misaada iliyotolewa ni sukari, mchele, unga, maharage, maji, dawa za usafi, khanga, mashuka ya watoto, ndala, mifagio, dawa za meno, mafuta ya kupaka, pedi za wanawake, nepi za watoto, maziwa ya watoto, vitabu vya dini ikiwemo Qur’an na Biblia pamoja na nguo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Gereza la Wanawake Segerea, SSP Hamida Mussa Matimba, ameishukuru TPSC kwa msaada huo akisema vitabu vya dini vitakuwa nguzo muhimu katika kuwajenga wafungwa kiimani na kuwasaidia katika mchakato wa mabadiliko chanya.
Alieleza kuwa gereza hilo linaendesha programu mbalimbali za mafunzo ya ufundi stadi ikiwemo ushonaji, upishi, ufyatuaji wa matofali, ujenzi, ufundi magari na umeme, akisisitiza kuwa lengo ni kuhakikisha kila anayeingia gerezani anatoka akiwa na mabadiliko chanya ya kiimani, kimaadili na kiujuzi ili aweze kujitegemea anaporejea uraiani.
Aidha, aliwahimiza wanawake kuwa na moyo wa kusamehe ili kupunguza migogoro inayoweza kuishia kwenye vyombo vya sheria, akitolea mfano wa migogoro ya madeni katika vikundi vya mikopo. Pia alitoa wito kwa wazazi kuwalea vijana, hususan mabinti, katika misingi ya maadili na kuwajenga kuridhika ili kuepuka tamaa zinazoweza kuwaingiza katika matatizo ya kisheria.
Meneja wa Sehemu ya Mafunzo kwa Njia ya Mtandao TPSC,Zena Hussein (kushoto) akikabidhi
Meneja wa Sehemu ya Mafunzo kwa Njia ya Mtandao TPSC,Zena Hussein akizungmza wakati kukabidhi misaada huo.











Post A Comment: