Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, amesema ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Kituo cha Kupokea na Kupoza Umeme wa Kilovoti 400 cha Iganjo mkoani Mbeya, ambao kwa sasa umefikia takribani asilimia 60 ya utekelezaji wake.
Mhe. Ndejembi ametoa kauli hiyo Machi 8, wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo unaotekelezwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) katika eneo la Iganjo jijini Mbeya ambao ni sehemu ya Mradi wa Njia kusafirisha Umeme kutoka mkoa wa Irunga hadi Mkoa wa Rukwa (TAZA).
“Kwa ujumla wake kazi hapa zinaenda vizuri sana. Niwapongeza Shirika la Umeme TANESCO kwa kazi ya usimamizi mzuri wa mradi huu,” amesema Mhe. Ndejembi
Akieleza faida za mradi huo amesema kuwa utaachangia kuimarisha hali ya upatikanaji wa umeme katika Mkoa wa Mbeya pamoja na mikoa jirani.
“Mradi huu utaongeza nguvu ya upatikanaji wa umeme kwa sababu kwa sasa Mkoa wa Mbeya unapata umeme kutoka kwenye njia ya kilovoti 220 lakini mradi huu utakua ni kilovoti 400. Wananchi watanufaika na mradi huu kwa sababu umeme utapoozwa na kusambazwa kwa Wananchi,” ameongeza Mhe. Ndejembi
Aidha, ameeleza kuwa serikali inayoongozwa na Rais wa awamu ya sita Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuwekeza katika miradi mikubwa ya kimkakati ya nishati ili kuimarisha hali ya upatikanaji wa umeme kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa Tanzania - Zambia (TAZA) Mha. Elias Makunga amesema mradi wa kituo cha Iganjo unaendelea vizuri licha ya changamoto ndogo zilizojitokeza katika hatua za usambazaji wa vifaa.
“Mradi wa kituo cha Iganjo uko asilimia 60 ya utekelezaji, ujenzi wa misingi umekamilika kwa asilimia 89. Upande wa usambazaji wa vifaa kutoka China tuko asilimia 89, lakini tumekuwa na changamoto kidogo katika upande wa upokeaji wa vifaa unaohusiana na kuboresha mfumo wa TRA,” amesema Mha. Makunga
Mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Iringa hadi Rukwa ukikamilika unatarajiwa kuwa miongoni mwa miradi muhimu katika kuimarisha Gridi ya Taifa na kuongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika katika ukanda wa Nyanda za Juu Kusini.





Post A Comment: