Na Mwandishi wetu -Dodoma


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Uratibu na Watu Wenye Ulemavu (SBUU) Mhe. Ummy Nderiananga amesema, Serikali itaendelea kuwaunga mkono watu wenye ulemavu ili wajikwamue kiuchumi.


Mhe. Nderiananga alisema  hayo wakati akikabidhi Cherehani kwa mkazi wa Mtaa wa Viwandani Bw. Eliah Ndayabunya mwenye ualbino  alipomtembelea Ofisini kwake Jijini Dodoma.

Alisema, amemkabadhi cherehani hiyo kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Watu Wenye Ulemavu) ili kumrahisishia shughuli zake za ushonaji kwa lengo la kujipatia kipato na kupunguza utegemezi.


“Tumefurahi tumempokea kijana wetu, alifika katika Ofisi hii kueleza shida yake ambapo alitaka kusaidiwa cherehani, hivyo kupitia Ofisi ya Waziri wa Nchi Mhe. William Lukuvi nimemkabidhi kifaa hiki  hatua ambayo ni kuonyesha utu na kuwathamini watu wenye ulemavu,” alisema Mhe. Nderiananga.


Pia, aliongeza kuwa juhudi hizo ni kushiriki falsafa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha watu wenye ulemavu hawaachwi nyuma katika shughuli za maendeleo.


Aidha, akitoa shukrani zake kwa Serikali mara baada ya kukabidhiwa Cherehani hiyo Bw. Ndayabunya alimshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Ofisi ya Waziri Mkuu inayoshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu kwa kundi hilo katika nyanja zote  za kiuchumi, kisiasa hata kijamii.


“Cherehani hii inaongeza kipato kupitia shughuli zangu za ufundi, namshukuru Mheshimiwa Rais na Ofisi hii ya Waziri Mkuu kwa sababu  kifaa hiki kitanitoa katika hali ya utegemezi maana tayari nina ujuzi ambao naenda sasa kuufanyia kazi,”alipongeza Bw. Ndayabunya.


*MWISHO*

Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: