Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI anayeshughulikia Elimu, Mhe. Reuben Kwagilwa, amewatoa hofu wazazi na walezi nchini kuwa Serikali imejipanga kikamilifu kuwapokea wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kuanzia Januari 2026, kwani imeandaa miundombinu ya kutosha itakayowahudumia wanafunzi wote watakaopokelewa.
Mhe. Kwagilwa ametoa kauli hiyo mkoani Lindi wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, ambapo alitembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Shule ya Msingi Likong’o, iliyopo katika Manispaa ya Lindi.
“Shule hii inakwenda kuongeza na kutimiza idadi ya shule 567 zilizojengwa nchini. Ukiacha shule hii, tayari zipo shule 566 zilizojengwa nchi nzima, na kwa hapa mkoa wa Lindi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameleta Shilingi Bilioni 114 kwa ajili ya kuimarisha sekta ya Elimu,” amesema Mhe. Kwagilwa.
Ujenzi wa Shule ya Msingi Likong’o ni sehemu ya miradi ya kijamii inayotekelezwa kupitia sera ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) chini ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), kwa kushirikiana na kampuni za Equinor na Shell, ambazo ni wadau wa maendeleo katika sekta ya mafuta na gesi.
Mhe. Kwagilwa amesema mradi huo umelenga kuboresha miundombinu ya elimu kwa watoto wa shule za msingi kwa kutoa mazingira salama, ya kisasa na bora ya kujifunzia, ikizingatiwa kuwa awali eneo hilo lilikuwa likikabiliwa na changamoto ya miundombinu ya elimu.
Ujenzi huo unahusisha vyumba vya madarasa na miundombinu ya kusaidia utoaji wa elimu bora kwa wanafunzi, ambapo thamani ya mradi huo inakadiriwa kufikia Shilingi Bilioni 1.2 za Kitanzania na Serikali imesisitiza kuwa hatua hii ni sehemu ya jitihada za kuwekeza katika elimu kwa maendeleo endelevu ya taifa.

Post A Comment: