Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amefanya ziara ya kushtukiza katika huduma ya mabasi ya mwendokasi ya Gerezani - Kimara, ili kujiridhisha na utoaji wa huduma mara baada ya Serikali kuelekeza huduma hiyo irejee katika jiji la Dar es Salaam.

Prof. Shemdoe ametumia fursa hiyo kusikiliza malalamiko ya wananchi wanaotumia usafiri wa Mwendokasi, ambapo wamelalamika juu ya uchache wa mabasi ya mwendokasi hatua iliyopelekea Prof. Shemdoe kumpigia simu na kumuelekeza Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (UDART) Bw. Pius Andrew Ng’ingo kuongeza mabasi ya mwendokasi ili yawahudumie wananchi.

Hatua hiyo ya Prof. Shemdoe kutembelea huduma ya mabasi ya mwendokasi imepokelewa vizuri na wananchi wanaotumia mabasi hayo, ambapo wamempongeza kwa kitendo chake cha kufanya ufuatiliaji ili kujiridhisha na huduma inayotolewa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI Mhe. Prof. Riziki Shemdoe mara baada ya kuapishwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza maelekezo ya Mhe. Rais ya kuwaletea wananchi tabasamu, hivyo ziara hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya kuhakikisha wananchi wanapata tabasabu kupitia huduma zitolewazo na mabasi ya mwendokasi.

Share To:

Post A Comment: