📍Ataimarisha upatikanaji wa huduma za afya katika zahanati
📍kuhakikisha vitongoji ambavyo havina Umeme, vinapata Nishati hiyo
📍 Kuimarisha uchumi wa mtu mmoja mmoja ikiwemo upatikanaji wa mikopo yenye riba nafuu
📍 Leng'ese aagiza viongozi wa CCM kata, tawi na shina, kutafuta kura za wagombea wa CCM
📍 Mwenyekiti wa UVCCM wilaya Aziza awataka wana-Kigombe kuchagua wagombea wa CCM
📍 Asha na George watia Nia Ubunge Muheza, wapanda jukwaani kusaka kura za CCM
Na Mwandishi Wetu, Muheza
MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Muheza kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Hamis Mwinjuma maarufu MwanaFA, ametaja vipaumbele vitatu endapo wananchi wa kata ya Kigombe watamchagua katika uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29 mwaka huu.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika mji wa Kigombe, MwanaFA alisema katika mambo aliyopanga kuyatekeleza endapo atachaguliwa tena, ni kusimamia mambo ya ustawi wa jamii ya watu wa Kigombe.
"Malengo yangu niliyokuwa nayo ndugu zangu wa Kigombe endapo mtanichagua ubunge, Kwanza nitaboresha na kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma za afya katika zahanati yetu" alisema.
MwanaFA ambaye ni Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, alisema atahakikisha anaiboresha zahanati ya Kigombe ili iwe na ubora wa upatikanaji wa huduma mbalimbali za afya kwa kiwango kikubwa.
Kipaumbele cha pili alichosema Zumbe wa mkoa wa Tanga, ni kuhakikisha vitongoji vitatu ambavyo havijapata Nishati ya Umeme, vitapatiwa katika mwaka ujao wa fedha.
Alisema wakati akiingia Kijiji cha Mtiti na vitongoji sita havikuwa na Umeme lakini Sasa vimebaki vitatu ambavyo navyo vitapatiwa Nishati hiyo.
Suala la tatu katika kipaumbele chake, MwanaFA alisema kuwa ataendelea kuwawezesha kiuchumi wananchi wa Kigombe ili mtu mmoja mmoja aweze kupiga hatua kiuchumi ikiwemo kuwapa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri.
Aliwashukuru wananchi wa Kigombe kwa kukiamini Chama Cha Mapinduzi (CCM) na hatimaye katika miaka mitano iliyopita walipata kiasi cha shilingi bilioni 2.8 kwa ajili ya miradi ya Maendeleo.
"Ipo sababu kwanini upinzani Kigombe umekufa, zipo sababu haukufa hivi hivi, nawashukuru sana kwa kukiamini Chama Cha Mapinduzi," alisema MwanaFA.
Alisema moja ya sababu ya upinzani kufa katika kata hiyo ni historia ya kata hiyo kupata fedha nyingi za miradi ya maendeleo kuliko wakati mwingine wowote ule.
"Tumekuwa na upinzani hapa Kigombe kwasababu mambo mnayotaka yafanyike hayajafanyika...Mnataka haki mnataka mambo yenu yafanyike," alisema na kutaja miradi mbalimbali ambayo imeletewa fedha katika kipindi cha mwaka 2020-2025.
MwanaFA alisema kwa upande wa mradi wa maji jumla ya shilingi bilioni 1.3 ililetwa katika kata hiyo kwa ajili ya mradi wa maji baada ya maeneo mengi kuchimbwa visima lakini wananchi wanapata maji yenye chumvi.
Alisema wataimarisha upatikanaji wa maji katika maeneo ya Chakalaboko, Mtiti na maeneo mengine ili huduma ya majisafi na salama yaweze kupatikana katika kata hiyo.
Alisema katika sekta ya afya zahanati ya Kigombe ilipatiwa kiasi cha shilingi milioni 120 ambayo ilisaidia kupatikana nyumba ya daktari na kuboresha miundombinu ya zahanati hiyo.
"Miaka mitano ijayo tutafanya upanuzi wa zahanati yetu lakini pia uwezekano wa kupata kituo cha afya, jambo mnalotakiwa ni kufanya subra ndugu zangu," alisema.
Katika elimu ya msingi na sekondari jumla ya shilingi milioni 129.3 zililetwa kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya shule pamoja na kuweka Umeme katika shule ya sekondari.
Kuhusu uvuvi MwanaFA alisema kwamba serikali ilileta boti sita zenye thamani ya shilingi milioni 727 ambazo zimeleta nema kwa wavuvi ambao wameweza kuongeza kipato chao cha Kila siku.
Kuhusu barabara alisema kiasi cha shilingi milioni 156 kililetwa kata hiyo kwa ajili ya kukarabati barabara ya Kigombe-Mtiti yenye urefu wa kilomita Saba ambapo iliweza kuwekewa changarawe.
Akizungumza maombi mbalimbali yaliyowasilishwa na mgombea udiwani wa kata hiyo Shahongwe Mgandi alisema Kila changamoto iliyopo katika Jimbo la Muheza ni kipaumbele chake, hivyo atazifanyia kazi.
Aliwataka wananchi wa Kigombe kumchagua kwa kura nyingi mgombea Urais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwa ameiheshimisha wilaya hiyo kwa kuleta miradi mingi katika kipindi cha miaka minne na nusu ya uongozi wake.
"Naomba kura za kishindo kwa Dkt Samia Suluhu Hassan, tumpeni kura nyingi ili tumtie moyo ametufanyia kazi nyingi katika wilaya yetu," alisema na kuongeza,
"Nichagueni na Mimi MwanaFA Hamis Mwinjuma, lakini pia diwani wenu pamoja na kwamba yupo pekee yake lakini mnatakiwa mumpigie kura za ndiyo,".
Awali Katibu wa CCM wilaya ya Muheza Simon Leng'ese aliwataka viongozi wa CCM wa kata hiyo kuhakikisha Kamati zao za ushindi zinapita kwa wananchi kwenda kuomba kura ili chama hicho kiweze kupata kura nyingi katika uchaguzi Mkuu ujao.
Meneja kampeni wa mgombea ubunge wa CCM katika Jimbo hilo, Aziza Mshakangoto na mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Muheza alisema kuwa wananchi wa Kigombe wanapaswa kujivunia kazi nzuri iliyofanywa na serikali katika kipindi kilichopita.
"Barabara hii ya Tanga Pangani ikikamilika mtaitumia kusafirisha bidhaa zenu za bahari kama mlikuwa mkisafirisha mara moja Sasa mtasafirisha mara nyingi zaidi," alisema.
Azazi alisema kuwa changamoto haziwezi kumalizwa kwa mara moja wananchi Wana hitaji kuwa wastahimilivu kwakuwa kilichofanyika pia ni hatua kubwa kwao.
George Semunga na Asha Wandi watia Nia ya ubunge katika Jimbo hilo, walipata nafasi ya kuwanadi mgombea ubunge na diwani lakini pia walimuombea kura Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwakuwa ni Rais aliyeitendea vema nafasi hiyo katika kipindi cha miaka minne na nusu.
Post A Comment: