Mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuimarisha sekta ya miundombinu ikiwa ni pamoja na barabara, reli na bandari kavu, ili kuongeza ufanisi wa usafirishaji na biashara kati ya Tanzania na nchi jirani.

Akizungumza leo Septemba 3, 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika eneo la Tunduma Mpakani, wilayani Momba mkoani Songwe, Dkt. Samia amesema tayari hatua za awali zimeanza kuchukuliwa katika barabara na reli zinazounganisha Tanzania na Zambia.

Ameongeza kuwa reli ya TAZARA pia iko kwenye mpango maalum wa ukarabati ili kuongeza kasi ya usafirishaji wa mizigo.

“Tumeshaanza taratibu za kukarabati na kuimarisha reli ya TAZARA. Lazima tuifanyie ukarabati ili mzigo uende kwa haraka. Hilo nalo lipo kazini maana tumeshasaini na Wachina ili kazi ianze,” amesema.

Katika hatua nyingine, Dkt. Samia amebainisha kuwa serikali yake inakwenda kukamilisha ujenzi wa bandari kavu kubwa yenye ukubwa wa ekari 1,800 katika kata ya Mpemba, Tunduma, ikiwa ni suluhisho la msongamano na kuegeshwa kwa malori barabarani.

Mgombea huyo wa CCM ameahidi kuwa miradi hiyo ni sehemu ya ajenda ya chama chake ya kuimarisha uchumi wa viwanda na biashara kimataifa kwa kutumia miundombinu ya kisasa.


Share To:

Post A Comment: