Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka wananchi wa Wilaya ya Uyui kujiamini kwa kile alichokiita “mafanikio yanayoonekana na yanayoendelea kujengwa kwa kasi” kupitia Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka 2025.

Akihutubia wananchi wa Uyui, Dkt. Samia amesema katika kipindi cha uongozi wake, Serikali ya CCM imefanikisha kukamilika kwa ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya hiyo, jambo lililochochea kuimarika kwa huduma za afya. Aidha, alibainisha kuwa miradi ya maji safi na salama imeboreshwa huku shule mpya za msingi na sekondari zikijengwa ili kuongeza fursa za elimu kwa watoto.

Katika sekta ya kilimo na mifugo, ameeleza kuwa upatikanaji wa mbolea za ruzuku umeongezeka, hivyo kusaidia kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara. Vilevile, Serikali imeimarisha usambazaji wa dawa za mifugo na kutoa elimu ya ufugaji bora kwa wafugaji wa Uyui.

“CCM haiahidi tu, bali inatekeleza. Tumekamilisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme, na sasa tupo kwenye hatua ya kuhakikisha zahanati mpya zinajengwa katika vijiji zaidi ya kumi, ikiwemo Hiari ya Moyo, Mhulidede, Mdalaigwe na Kalemela. Pia tunakamilisha majengo ya mama na mtoto, wodi za wazazi na vituo vya afya,” alisema Dkt. Samia.

Kwa upande wa miradi mipya, Dkt. Samia ameahidi upanuzi wa mradi wa maji wa Ziwa Victoria, ujenzi wa bwawa na skimu za umwagiliaji katika vijiji mbalimbali, pamoja na barabara za changarawe na lami kwa ajili ya kuchochea uchumi wa wananchi.

Share To:

Post A Comment: