Na. James K. Mwanamyoto - Morogoro

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Bw. Adolf Ndunguru amesema Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejikita katika kukuza uchumi kupitia viwanda, biashara na uwekezaji ili kila Halmashauri iweze kutoa mchango halisi katika kuongeza thamani ya mazao, kutoa ajira kwa wananchi, na kukuza mapato ya ndani.

Katibu Mkuu Ndunguru amesema hayo leo mjini Morogoro katika Ukumbi wa Edema, wakati akifungua Mafunzo ya Uwekezaji na Viwanda kwa Wakuu wa Sehemu za Viwanda, Biashara na Uwekezaji wa Mikoa na Wakuu wa Divisheni za Viwanda, Biashara na Uwekezaji wa Halmashauri.

Bw. Ndunguru amesisitiza kuwa, Ofisi ya Rais-TAMISEMI itaendelea kutoa msaada wa kitaalam na uratibu ili kuhakikisha inatimiza dhamira ya Serikali ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na ya uchumi wa kati wa juu ambayo inayotoa ajira kwa vijana. 

Bw. Ndunguru amesema, maendeleo ya viwanda, biashara na uwekezaji hayawezi kupatikana kimiujiza kwani yanahitaji uongozi makini, mipango madhubuti na ushirikiano wa dhati kati ya Serikali Kuu, Serikari za Mitaa na Sekta Binafsi na wananchi na ndio maana TAMISEMI imeandaa mafunzo ya kuwajengea uwezo wataalam wa sekta wa sekta hizo.

“Nawasisitiza Wakuu wa Divisheni ya Viwanda Biashara na Uwekezaji kuingiza masuala ya kisekta kwenye Mpango Mkakati ya kila Mkoa na halmashauri, kwa kuzingatia Ilani ya Chama kitakachukuwa madarakani na Dira ya Maendeleo 2050,” Bw. Ndunguru amehimiza.

Bw. Ndunguru ameongeza kuwa, Serikali inatarajia mara baada ya mafunzo hayo kukamilika, wataalam hao watakwenda kusimamia kwa ufanisi sekta ya viwanda, biashara na uwekezaji ili kuleta maendeleo ya kiuchumi, ikiwa ni pamoja na kubadilishana uzoefu wa mbinu bora za kuvutia uwekezaji.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Serikali za Mitaa Sehemu ya Maendeleo ya Jamii na Utawala Bora Bw. Stephen Motambi amesema Ofisi ya Rais-TAMISEMI imeandaa mafunzo hayo ya siku mbili kwa wataalam hao waliopo kwenye ngazi ya msingi kwa lengo la kuwajengea uwezo kiutendaji ili waweze kuvutia na kuwapokea wawekezaji katika eneo la viwanda.

Aidha, Bw. Motambi amesema kuwa mafunzo hayo yatatumika kuwajengea uwezo wa maboresho yaliyofanyika kwenye mfumo wa TAUSI unaotumika kukusanya mapato ya halmashauri kupitia malipo ya huduma mbalimbali kama vile Leseni za biashara, Vibali vya ujenzi, uvuvi, malipo ya kodi za majengo na ununuzi wa viwanja.

Katika mafunzo haya ya siku mbili washiriki watapitishwa katika mada za uwekezaji, usimamizi wa viwanda, mabadiliko ya sheria leseni za biashara ikiwa ni pamoja na mada ya maboresho ya mfumo wa TAUSI.









Share To:

Post A Comment: