Na Mwandishi Wetu
WIZARA ya Nishati imesisitiza kuwa imeweka mkakati wa kuhakikisha wananchi wote wanatumia nishati safi ya kupikia na kuachana na matumizi ya kuni na mkaa ambayo yamekuwa na madhara ya kiafya na kimazingira huku ikiwapongeza wadau wakiwemo Oryx Gas kwa kushiriki kikamilifu katika kufanikisha mkakati huo.
Hayo yameelezwa jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Nishati Safi ya Kupikia kutoka Wizara ya Nishati, Nolasco Mlay wakati wa uzinduzi wa kampeni ya maalum ya Gesi Yente na Oryx Gas yenye lengo la kuhamasisha matumizi ya nishati safi yakupikia kwa Watanzania wote.
“Usipotumia nishati safi ya kupikia kuna madhara makubwa kiafya na kimazingira, tunaweza kuona wenyewe siku hizi watu wengi wamekata miti kwasababu wanatumia kwa ajili ya kupikia mkaa na kuni.
“Hivyo tunahama kutoka kutumia nishati isiyo safi ya mkaa na kuni na kuanza kutumia nishati safi ya kupikia, ndio maana wadau kama ORYX GAS na wadau wengine wanashirikiana na Serikali ambayo imekuja na mkakati ifikapo 2034 asilimia 84 ya Watanzania tuwe tumehamia kwenye nishati safi ya kupikia.
“Na ukweli ORYX wanatusaidia sana kwasababu wako Tanzania nzima na mpango wao ni kuendelea kushiriki kikamilifu kuhakikisha mkakati wetu ifikapo 2034 wananchi asilimia 84 wawe wanatumia nishati safi ya kupikia na tuachane na matumizi ya kutumia kuni na mkaaa.
“Kama Serikali tukisaidiana na wadau kama ORYX tunahakikisha tunaweka ruzuku kwenye gesi ili kila mwananchi aweze kumudu kununua gesi,kutumia na kumudu gesi inapoisha.Wananchi waelewe tunapozungumzia nishati isiyo safi ndio nishati ukitumia inakuathiri kiafya,”amesema Mlay.
Amesisitiza Serikali pia inamkakati wa kupunguza kodi katika bidhaa za nishati safi kwani kodi inapokuwa juu na bei ya bidhaa hizo inakuwa kubwa huku akifafanua tayari kuna mkakati ambao umeanza na kuna rasimu ambayo imeshapelekwa kwa ajili ya mchakato utakaowezesha bidhaa za nishati safi ya kupikia zishuke bei ili kıla Mwananchi amudu.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Gas Tanzania Araman Benoit amesema wameendelea kuwahamasisha Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia kwani tafiti zinazonesha maelfu ya familia bado zinategemea kuni,mkaa na mafuta ya taa kwa kupikia hali inayoongeza magonjwa katika Mfumo wa hewa na uharibifu wa mazingira.
“Tunaishi kipindi ambacho afya ya jamii na mazingira yetu inahitaji kulindwa zaidi ya wakati mwingine wowote. Kuna maelfu ya familia bado hutegemea kuni, mkaa, na mafuta ya taa kwa kupikia, hali inayoongeza hatari ya magonjwa ya njia ya hewa, uharibifu wa mazingira, na gharama kubwa za maisha kwa muda mrefu.
“Kupitia kampeni ya Gesi Yente, tunalenga kurejesha mitungi ya gesi iliyopakiwa majumbani na isiyotumika sokoni, na kuirudisha kwenye matumizi. Mitungi hii siyo ya kupuuzwa ni rasilimali muhimu ambayo inaweza kusaidia familia nyingi kupikia kwa usalama, kwa haraka, na kwa gharama nafuu.”
Pia amesema kupitia kampeni hiyo Oryx Gas itakuwa inatoa zawadi mbalimbali kwa washindi katika kampeni hiyo na miongoni mwa zawadi zitakazotolewa ni kama vile pikipiki, baiskeli, seti ya sufuria, mabegi ya shule.
Pamoja na hayo amesisitiza huu ni wakati wa kuamka kama taifa na kumuunga mkono kiongozi wetu wa taifa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kuipeleke nchi viwango vingine kwenye suala la nishati safi.
“Tunawahimiza Watanzania wote kama una mtungi wa gesi ulioiacha nyumbani ni wakati wa kuuleta tena sokoni, ni wakati wa kuutumia tena na ujishindie zawadi kemkem.Na kwa wale ambao bado hawajaanza kutumia gesi tunawahamasisha kuchukua hatua na waanze kutumia gesi.Tunaweza kujenga taifa linalotumia nishatisafi, salama, na rafiki kwa mazingira.”
Post A Comment: