Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amekagua mradi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovolti 400 kutoka Chalinze hadi Zuzu Dodoma na kueleza kutoridhishwa kwake na utekelezaji wa mradi huo ambao ulipaswa kuwa umefikia asilimia 31 lakini kwa sasa umefikia asilimia 24 tangu kuzinduliwa kwake Novemba mwaka 2024.
Hali ya kusuasua kwa mradi imebainika wakati Dkt. Biteko akikagua mradi huo katika Kijiji cha Manchali wilayani Chamwino mkoani Dodoma tarehe 20 Agosti 2025 ambapo Dkt. Biteko amemuagiza mkandarasi kampuni ya TBEA ya China kuhakikisha kuwa anafidia muda wa kazi uliopotezwa wa asilimia Saba ili mradi ukamilike kwa wakati kutokana na umuhimu wake nchini.
Mwezi Novemba, 2024 Serikali ilikubaliana na mkandarasi kuwa mradi huo ufanyike ndani ya miezi 19 tu badala ya miezi 22 kwani wakati mradi unazinduliwa tayari kazi kubwa za awali zilikuwa zimeshafanyika ikiwemo za upembuzi yakinifu na utoaji wa maeneo.
“ Leo ni miezi saba imepita tangu tuzindue mradi sawa na asilimia 32 ya muda wote tuliokuwa tunahitaji kutekeleza mradi huu, na tulitegemea mradi kwa sasa ufikie asilimia 31 lakini katika hali ya kushangaza mradi umefikia asilimia 24 tu jambo ambalo halikubaliki.” Amesema Dkt. Biteko
Dkt. Biteko ameeleza kuwa, sababu zilizotolewa na Mkandarasi za kuchelewesha mradi ikiwemo ya wananchi kugoma kutoa maeneo kwa madai ya fidia na kukutana na miamba katika mkuza wa mradi hazikubaliki kwani wananchi hao wana haki na lazima walipwe fidia.
Kutokana na hali hiyo, ameagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kutumia mapato yake ya ndani kulipa fidia wananchi waliopisha mradi.
Dkt. Biteko ametanabaisha kuwa mkandarasi alishaagizwa asiutekeleze mradi huo kwa mazoea kutokana na umuhimu wake kwani kwa sasa miundombinu inayosafirisha umeme kwenda Dodoma kutoka mradi wa Julius Nyerere (JNHPP) kupitia kituo cha Chalinze inabeba umeme kidogo kwa takriban megawati 240 tu ambayo ni sawa na mashine moja tu kati ya mashine 9 za JNHPP hivyo njia hiyo mpya ya umeme ya kV 400 inayojengwa ni muhimu.
Amesisitiza kuwa njia mpya ya umeme ya kV 400 ni muhimu kwani katika Mkoa wa Dodoma mahitaji ya umeme yanaongezka kila siku huku mkoa huo pia ukiwa ni kitovu cha usambazaji umeme katika mikoa yote ya Magharibi ikiwemo Singida, Tabora, Shinyanga Mara na Kigoma ambayo inategemea utulivu wa umeme katika Mkoa wa huo na kwamba Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan alishaagiza kuwa mradi huo usichezewe hivyo Mkandarasi ahakikishe kuwa anaupa umakini mkubwa.
Kutokana na mradi huo kuwa nyuma katika utekelezaji, Dkt. Biteko amemuagiza Mkandarasi kuja na mpango mpya wa utekelezaji wa kazi ukiwemo wa kufidia muda uliopotezwa ambapo ametoa siku nne mpango wa fidia ya muda uwasilishwe kwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati.
Vilevile, Dkt. Biteko ameagiza mkandarasi kuongeza nguvu kazi ya watu ili minara 917 ya umeme inayopaswa kujengwa kwenye mradi huo ijengwe kwani kwa sasa mkandarasi amechimba takriban mashimo 100 tu kwa ajili ya usimikaji wa minara. Pia amemtaka Mhandisi mshauri wa mradi kuhakikisha anasimamia mradi huo kwa ufanisi na aeleze ukweli pale anapoona kuwa hauendi sawa.
Aidha amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, kutengeneza timu itakayoungana na TANESCO kuusimamia mradi huo na kila wiki taarifa itolewe kuwa umefikia wapi.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amewaasa Wananchi kutozuia utekelezaji wa miradi pale inapopita kwenye maeneo yao na Serikali kwa upande wake itahakikisha kuwa wanapata haki wanazostahili kwani Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshaelekeza kuwa hataki wananchi wafanyiwe dhuluma ambapo wasaidizi wake wanahakikisha kuwa agizo hilo linatekelezwa.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema mradi huo wa usafirishaji umeme wa kV 400 kunaenda kuifanya Dodoma kuwa kitovu cha usambazaji umeme nchini.
Aidha, ameahidi kuyasimamia maelekezo yote yaliyotolewa na Dkt. Biteko ya kuhakikisha kuwa mradi huo unakamilika kwa wakati ili kuwezesha umeme huo utakaofikishwa Dodoma, kusambazwa pia kwenye maeneo mengine nchini.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange amesema Mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma unakusudia kusafirisha umeme wote unaozalishwa kutoka katika Bwawa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere (Megawati 2,115) na kuingiza kwenye gridi ya Taifa kisha kuufikisha kwenye maeneo yote yenye mahitaji ya umeme.
Amesema mkataba na mkandarasi kampuni ya TBEA ulisainiwa mwaka 2024 na mradi kuanza kutekelezwa mwezi Novemba 2024 ambapo mkandarasi ameshalipwa awamu ya kwanza ya malipo ambayo ni shilingi za kitanzania bilioni 107 na mhandisi mshauri ameshalipwa asilimia 15 ya malipo yake.
Ameeleza kuwa maagizo yote yaliyotolewa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati yatafanyiwa kazi ikiwemo ya kuhakikisha kuwa mradi unakamilika mwezi Juni au kabla ya Juni 2026 kwa mujibu wa mkataba.
Aidha, Ameishukuru Serikali chini ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa shilingi bilioni 513 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo ambao utakuwa na urefu wa kilometa 345 na kuhusisha minara ya umeme ipatayo 917 kutoka Chalinze mkoani Pwani hadi Zuzu mkoani Dodoma.
Post A Comment: