NA EMMANUEL MBATILO DAR ES SALAAM
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeendela kutoa hamasa kwa washiriki wa Tuzo za Ubora kwa mwaka 2025/26 kufanya maombi ambapo wadau wameaswa kuzingatia mwisho wa tarehe ya kutuma maombi ya ushiriki ambayo ni Julai 31, 2025, kwa vipengele vyote vilivyotangazwa, katika pande zote za Muungano wa Tanzania.
Tuzo hizo zinashindaniwa katika vipengele saba ikiwemo: Kampuni Bora ya Mwaka (kwa mjasiriamali na kampuni kubwa), Bidhaa Bora ya Mwaka (kwa mjasiriamali na kampuni kubwa), Mtoa Huduma Bora wa Mwaka (kwa mjasiriamali na kampuni kubwa), Muuzaji Bora wa Bidhaa za kilimo Nje ya Nchi (kwa mjasiriamali na kampuni kubwa) Muuzaji Bora wa Bidhaa Mchanganyiko Nje ya Nchi (kwa mjasiriamali na kampuni kubwa), pamoja na Mtu Binafsi Aliyechangia Masuala ya Ubora.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 29, 2025 Jijini Dar es Salaam, Afisa Udhibiti Ubora wa TBS, Athumani Kisumo, amesema dhima kuu ya tuzo hizo ni kutambua kazi kubwa ya wadau katika kuendeleza masuala ya ubora na kuhamasisha wazalishaji na watoa huduma kuzingatia ubora wakati wa uandaaji wa bidhaa na kutoa huduma ili ziweze kufikia viwango vya kitaifa na kimataifa na kupata masoko katika kanda za Africa Mashariki (EAC) na Kusini mwa African (SADC).
"Kupitia jukwaa hili, washiriki watapata fursa ya kutambulisha bidhaa na huduma zao hapa nchini na hata kuvuka mipaka ya kibiashara katika ukanda wa Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Kusini mwa Afrika (SADC) ambapo washiriki watashindanishwa na wengine na kuweza kujitangaza katika Nchi zaidi ya 24" amesema Kissumo.
Kisumo amebainisha kuwa kampuni zinazotaka kushiriki lazima ziwe zimesajiliwa nchini Tanzania na ziwasilishe taarifa za mafanikio yao huku wakionisha na masuala ya kuimarisha ubora wa bidhaa au huduma zao, kutumia picha pamoja na grafu inayoonyesha mafanikio hayo na mikakati na kuonesha fursa ambazo wametengeneza au ajira kutokana na kuimarisha ubora katika kuzalisha au kutoa huduma.
Aidha, amesema kuwa washindi wa mashindano yaliyopita ya 2024/25 wameweza kushindanishwa katika kanda ya Jumuia ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika (SADC) na kushinda tuzo mbalimbali.
Tanzania katika mashindano ya ukanda wa SADC yanayoendelea huko Madagascar Washindi wanaoiwakilisha Tanzania walifanikiwa kupata ushindi katika vipengele vitatu kama ifuatavyo; Mshindi wa kwanza kwa mtu aliyetoa mchango wa kuboresha miundombinu ya Ubora ya SADC – Prof. Bendatunguka Tiisekwa – Sokoine University of Agriculture, Mshindi wa pili wa SADC tuzo ya Kampuni bora ya Mwaka ya SADC (Kampuni Kubwa) – SAID SALIM BAKHRESA AND COMPANY LTD, Mshindi wa tatu wa SADC tuzo ya Kampuni bora ya Mwaka ya SADC (Mjasiriamali) – CAPS Tanzania LTD, Mshindi wa tatu wa SADC tuzo ya bidhaa bora ya mwaka (Kampuni kubwa) – Sukari ya Bwana Sukari kutoka kiwanda cha Kilombero Sugar Company Limited na Mshindi wa tatu wa SADC tuzo ya Muuzaji bora wa bidhaa nje ya nchini (East Cost Oil and Fats Ltd). Hatua hii inathibitisha umuhimu wa tuzo hizo katika kukuza biashara kimataifa na kikanda yaani wa Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Kusini mwa Afrika (SADC).
TBS, kwa niaba ya Wizara ya Viwanda na Biashara, Jukwaa la Sector Binafsi (TPSF), ZBS pamoja na taasisi nyingine, zimekuwa ikiandaa tuzo hizo kwa misimu sita mfululizo tangu kuanzishwa kwake hapa Tanzania zikiwa na lengo la kutambua na kuthamini kuhudi za wadau katik kukuza ubora wa bidhaa na huduma sambamba na kuongeza wigo wa masoko ya ndani na nje ya nchi.
Post A Comment: