Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Samwel M. Maneno amefanya mazungumzo na Ujumbe kutoka Kampuni ya Kimataifa ya Mawakili ya Curtis ( Curtis, Mallet-Prevost,Colt&Mosle LLP Law firm) kwa nia ya kuanzisha fursa za ushirikiano katika maeneo mbalimbali kati ya Kampuni hiyo na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Naibu Mwanasheria Mkuu amezungumza na ujumbe huo tarehe 30 Julai, 2025 kwa njia ya mtandao, ambapo alianza kwa kuwashukuru Kampuni ya Mawakili ya Curtis kwa utayari wao wa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kuwajengea uwezo Mawakili wa Serikali katika maeneo mbalimbali ya Sheria.

Akizungumza wakati wa kikao hicho, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali alieleza kuwa kwa sasa Tanzania imekuwa ikitekeleza miradi mikubwa katika Sekta mbalimbali ikijumuisha Sekta ya Miundombinu, Uchukuzi, Nishati, Madini, Mawasiliano, Biashara na Uwekezaji.

Aidha, akizungunzia eneo la Uwekezaji, Mhe. Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameelezea dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kufungua fursa za Uwekezaji, hatua ambayo imeiwezesha Tanzania kuwa kituo bora cha Uwekezaji barani Afrika.

"Nchi yetu kwa sasa inafunguka zaidi katika eneo la Uwekezaji, na hii inatokana na maboresho makubwa ya kisera , mazingira wezeshi ya Biashara na Ushirikiano mkubwa na sekta binafsi hususan katika sekta za kibiashara, nishati, miundombinu yanayoendelea kufanywa na Serikali ya Awamu ya Sita, hivyo ninapenda kuwakaribisha kushirikiana nasi.'. Amesema Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali

Aidha, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali alisisitiza kuwa kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na nchi yetu katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati, kuna umuhimu mkubwa kwa Mawakili wa Serikali kujengewa uwezo wa kitaaluma wa kimataifa katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na majadiliano, usimamizi wa mikataba, utatuzi wa migogoro na kushikishwa katika Kampuni kubwa za uwakili duniani.

Akizungunza kwa niaba ya Kampuni ya Mawakili ya Curtis, Bi. Lise Johnson aliipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuona umuhimu wa kuongeza ujuzi kwa Mawakili wa Serikali na kuahidi ushirikiano katika eneo hilo kulingana na uzoefu mkubwa walionao katika nyanja mbalimbali za Sheria.

Aidha, amezungumzia uzoefu walionao katika nyanja mbalimbali za Sheria ikiwa ni pamoja na maeneo ya Ushindani, uendeshaji wa mashauri, usuluhishi wa migogoro, uwekezaji na biashara, ulinzi wa taarifa, faragha na mtandao, Fedha, Hakimiliki, Dhamana na Mtaji, Kodi, majadiliano ya Mikataba, Mikataba ya Ujenzi, Nishati, Mafuta na Gesi, na Maktaba Mtandao( e- library) .

Kampuni ya Curtis Law Firm ni Kampuni ya Kimataifa yenye Ofisi zake nchini Marekani, Amerika ya Kusini, Ulaya, na Mashariki ya Kati ikiwa na uzoefu wa muda mrefu katika maeneo ya Sheria na imekuwa ikishirikiana na nchi zinazoendelea kutoa msaada katika maeneo mbalimbali ikiwepo uendeshaji wa mashauri kwenye Mahakama za kimataifa pamoja na Mabaraza ya Usuluhishi ya Kimataifa ( International Arbitration Tribunals).

Miongoni mwa nchi zinazoendelea ambazo Kampuni hiyo imefanya kazi nazo ni Uganda, Nigeria, Cameroon, Panama, Colombia na Argentina.

Kikao hicho kilichoongozwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kilihudhuriwa pia na Mkurugenzi wa Mikataba na Makubaliano Bi. Sia Mrema, Wakili wa Serikali Mkuu Bi. Felista Lelo, Wakili wa Serikali Mkuu Bi. Catherine Paul na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Bi. Leila Muhaji.
Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: