Mbunge wa Jimbo la Mkuranga na Waziri wa Ujenzi Mhe. Abdallah Ulega amesema kwa kipindi cha miaka minne ya Rais Samia Suluhu Hassan, sekta ya Elimu kwenye Jimbo lake imeimarika zaidi, akitangaza pia ujio wa shule ya Sekondari ya Ufundi ambapo Bilioni 6 zimetolewa kukamilisha ujenzi wake utakaohusisha Majengo takribani 52.

Ulega amebainisha hayo leo Jumapili Juni 08, 2025, wakati akijibu maswali ya wanahabari Jijini Mwanza kwenye Mdahalo wa pamoja wa #MamaNiMjenzi, akibainisha kuwa dhamira njema ya Rais Samia imeondoa pia michango ya ujenzi wa miundombinu ya shule iliyokuwa ikilazimishwa kulipwa na wazazi.

"Mimi ni Mbunge na Jimboni ni diwani pia, nimekuwa Mkuu wa Wilaya Lindi kwa takribani miaka minne kasoro, unajua zamani unaenda baraza la Madiwani mpaka Bungeni, mnatumia muda mwingi diwani, Mbunge analilia darasa moja tu. Diwani anakasirika kabisa mwaka wa tatu hajapata darasa,leo tumejengewa madarasa huko Majimboni ambayo hatukuwahi kuota na michango ya wazazi kwaajili ya ujenzi imeisha kabisa." Amesema Mhe. Ulega.

Amezungumzia pia maboresho makubwa katika sekta ya Afya, akisema  wakati anaingia madarakani kama Mbunge, Jimbo lake lilikuwa na zahanati 14 pekee na leo zimefikia 58 zenye kutoa huduma kwa wananchi huku nyingine takribani 50 zikiwa kwenye hatua mbalimbali za za ukamilishwaji wake, lengo likuwa ni kila Kijiji kuwa na Zahanati yake.

Waziri Ulega ameeleza pia kuhusu huduma ya nishati, akibainisha kuwa Mwaka 2015 huduma hiyo ilipatikana Mkuranga Mjini pekee na miaka Kumi baadae Vijiji vyote 125 vinavyounda wilaya ya Mkuranga vinanufaika na huduma ya umeme chini ya serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Share To:

Post A Comment: