SHIRIKA la Grumeti Fund kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii imeendelea kuwa msaada kwa ukuaji kifkra kwa vijana wa kike na kiume Wilayani Serengeti kwa kuwaleta pamoja wanafunzi wa kike zaidi ya 900 na wakiume 810 kutoka katika shule za sekondari Mugumu na Sedeko zilizopo wilayani Serengeti ili kujadili namna bora ya kujenga jamii yenye ushirikiano wa pamoja kati ya vijana wa kike na kiume na hatimae kujenga jamii yenye usawa miongoni mwa vijana wa jinsia zote.
Akizungumza katika kongamano lililofanyika kwa siku mbili katika shule ya sekondari Mugumu na kuwakutanisha wanafunzi wa kike na kiume kutoka shule za sekondari Mugumu na Sedeko, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii kutoka Grumeti Fund Bi. Frida Mollel kwa nyakati tofauti amewataka vijana wa kike na wa kiume kutambua majukumu yao na nafasi zao katika jamii sambamba kuweka kipaumbele kwenye mambo ya msingi nafasi na kuacha kushughulika na mambo yasiyo ya msingi.
"Tuachane na mambo yasiyofaa ili tuweze kuyapa nafasi mambo ya msingi kuweza kuchukua nafasi katika vichwa vyetu, tunakosea kushughulika na mambo yasiyo na maana na tukayaacha yale yenye msaada kwetu kwa kuiga baadhi ya vitu ambavyo sio utamaduni wetu kwa hali hii hatutafika popote labda Mungu aingilie kati, Niwatie moyo sasa kuwa bado hamjachelewa bado mnayonafasi ya kubadilika na kuwa vijana wenye kutegemewa na familia zenu kama mkimtanguliza Mungu na ndio maana sisi Grumeti Fund kwa kutambua umuhimu wenu tumekuja kuwatia moyo kuwa unaweza kuwa mtu yeyote endapo utajitambua na kusoma kwa bidii na kumtanguliza Mungu katika kila jambo, tambueni kuwa mkisoma kwa bidii na kupata maarifa na ujuzi ndivyo vitu vitakavyokuokoa katika dunia hii", alisema Bi. Frida
Aidha, Bi. Frida ametoa msisitizo kwa vijana hao kuwa mstari wa mbele katika kukataa na kupinga mila na desturi za kigeni zinazoenda kinyume na maadili na chukizo kwa Mungu kwa kuwa na msimamo na maamuzi kwani ndio msingi wa kutotumbukia katika vishawishi vya dunia ya utandawazi.
Katika kongamano hilo shirika la Grumeti Fund imetoa Mipira na jezi za michezo Kwa shule zote mbili zilizoshiriki kwa wanafunzi wa kiume na kutoa msaada wa taulo za kike zinazoweza kutumika kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu (reusable pads) kwa wanafunzi wa kike zaidi ya 900 zenye thamani ya Shilingi 15,810,000 katika shule za sekondari Mugumu na Sedeko.
Naye mgeni rasmi katika makongamano hayo Mchungaji anayehudumia idara ya vijana katika kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Emmanuel Samuel Sitta kutoka mkoani Mwanza amewataka vijana hao wa kiume na wakike kujitambua na kutambua thamani yao sambamba na kuweka dira ya maisha yao mbele ili kuepuka changamoto za kimaisha huko baadae, huku akiwataka kumfanya Mungu kuwa mtatuzi wa changamoto zao na kuepuka ushawishi.
"Mfanye Mungu kuwa mtetezi wako katika kila jambo gumu lililokosa majibu, niwaambie kuwa ukimcha Mungu utaepuka mambo mengi mabaya, hata sisi tulivyo hivi ni kwasababu tuliwekeza katika kumcha Mungu na bado tunamtegemea yeye hadi sasa, bila Mungu dunia na tamaa zake zitakumeza. Ili kufanikiwa katika masomo yako jitahidi sana kuwa na hofu ya Mungu pamoja na kuwekeza katika masomo yenu. Jiepusheni na marafiki wabaya na mambo yasiyo na tija", alisema Mchungaji Emmanuel.
Kwa upande wake mkufunzi kutoka chuo cha Afya Kisare Mwl. Restuda Murutta akitoa Elimu ya uzazi kwa wanafunzi wa kike amewaasa kuzingatia usafi wawapo katika siku za hedhi na kuwataka kuzitumia taulo za kike zilizotolewa na Grumeti Fund kwa usahihi sambamba na kuepuka vishawishi vitakavyo waingiza katika kufanya mapenzi katika umri mdogo na mwisho kupelekea ndoa za utotoni.
“Usafi wakati wa hedhi ni muhimu sana kwani utaepuka magonjwa mbalimbali, lakini pia inasikitisha binti anaumri chini ya miaka 18 ameshaanza kujiingiza kwenye mahusiano ya ngono kitu ambacho sio salama, kabla ya kuingia kwenye mambo hayo kwanza jiulize je ni umri sahihi wa kuingia kwenye mambo hayo ukishapata jibu acha", alisema Bi. Restuda
Nao miongoni mwa wanafunzi wa kike na kiume waliopata mafunzo wameishukuru kampuni ya Grumeti Fund kwa namna wanavyowajali na kuwathamini vijana wa kike na kiume katika kujenga jamii bora yenye usawa na kuahidi kuyaweka katika vitendo mafunzo hayo na kusambaza elimu kwa wengine.
Kwa takribani miaka nane kampuni ya Grumeti Fund imekuwa ikitoa elimu ya kijinsia kwa wanafunzi wa kike na kiume katika shule za sekondari mbalimbali Wilayani Serengeti na Bunda ambapo tangu mwaka 2017 hadi awamu hii ya pili ya kongamano hili kwa Mwaka 2025 imefanikiwa kutoa elimu ya kijinsia kwa wasichana 17, 303 na kutoa jumla ya taulo 17,303 kwa kila binti anayeshiriki mafunzo hayo, huku ikifanikiwa kutoa mafunzo kwa wavulana zaidi ya 8,850 tangu mwaka 2021 hadi awamu hii ya pili ya kongamano la Mwaka 2025 na kutoa zawadi za jezi na mipira kwa kila shule iliyoshiriki kwenye kongamano.
Post A Comment: