Na Amani Nsello- MOI

Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) inatarajia kuendesha kliniki maalum ya kibobezi ya matibabu ya mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba  kwa mwaka 2025.

Hayo yamesemwa leo Ijumaa Juni 27, 2025 na Meneji Uhusiano wa MOI, Bw. Patrick Mvungi katika mkutano na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Mikutano uliopo katika taasisi hiyo.

Bw. Mvungi amesema Taasisi ya MOI itashiriki maonesho hayo kwa namna ya tofauti na miaka mingine ambapo madaktari bingwa wabobezi wataendesha kliniki maalum ya mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu.

"Tutakuwa na kiliniki maalum ya madaktari bingwa wabobezi wa mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu, ambapo wananchi watahudumiwa pale kwenye Viwanja vya Sabasaba" amesema Bw. Mvungi na kuongezea

"Tofauti na miaka mingine ambapo tulikuwa tukionesha huduma zetu tunazozitoa MOI  tumeona ni vyema kuzisogeza huduma zetu kwa wananchi"

Pia, Bw. Mvungi amesema kuwa gharama ya kumuona daktari bingwa itakuwa shilingi elfu tano (5,000) na kipimo cha ultra sound kitakuwa elfu kumi (10,000).

Kwa upande wake, Daktari bingwa mbobezi wa upasuaji wa mifupa MOI, Dkt. Tumaini Minja ametoa wito kwa wananchi kutumia fursa hiyo adhimu kufika katika banda namba 12 la MOI kwa ajili ya kupata huduma hizo za kibingwa .

Pamoja na mambo mengine Dkt. Minja amsema kutakuwa na madarasa maalum ya lishe bora ambapo wananchi watapewa elimu bure kuhusu lishe bora.

Pia, Dkt. Minja amesema MOI itatoa elimu na huduma za mazoezi tiba kwa wananchi ikiwa ni pamoja na mafunzo ya mitindo bora ya maisha ili kujiepusha na maumivu makali ya mgongo ambayo ni changamoto kwa watu wengi.



Share To:

Post A Comment: