Na Egidia Vedasto, Msumba News
Katika mafunzo ya Mawakili wa serikali yaliyofanyika Jijini Arusha, wamekumbushwa kurudi darasani kuongeza maarifa katika taaluma yao ili waweze kuisaidia nchi juu ya mikataba ya kimataifa.
Akifunga mafunzo hayo Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Eliakim Maswi amesema yuko tayari kuunga mkono Mawakili kwenda kusoma nje ya nchi ili kuhakikisha wanapatikana Mawakili wenye ubobezi na weledi katika sheria za masuala ya mikataba ya kimataifa, na mambo mengine nyeti watakaoitetea serikali na rasilimali zake.
Aidha amewataka kuzingatia usalama wa taarifa zao, matumizi sahihi ya teknolojia, na kuwahudumia wananchi kwa kuzingatia haki. Pia amewataka kuwa na maamuzi magumu katika kuchukua hatua pale wanapogundua mambo hayaendi sawa.
"Tunahitaji Mawakili wenye Dira ya kimkakati kwa kuzingatia misingi ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiutamaduni, Nyinyi ni watetezi wa maslahi ya umma na serikali katika utekelezaji wa majukumu ya kikatiba, utekelezaji wa haki iliyo bora, utungaji wa sheria, ulinzi wa amani na mikataba ya umma katika kuielekea Dira ya Taifa 2050 inayotaka maendeleo ya uchumi wa juu yakiendana na mabadiliko ya kidigitali" amesema Maswi.
Hata hivyo amesisitiza Mawakili wa serikali kuwa na nidhamu ya kazi, maadili ya kitaaluma, afya ya akili na kuepuka uzembe kazini pamoja na vitendo vya rushwa.
Kwa upande wake Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Alice Mtulo amesema kupitia mafunzo waliyopatiwa kwa siku tatu yamewapa mbinu za kisasa zitakazowawesha kufanya kazi kwa tija zaidi kwa kutumia teknolojia na kudumisha ustawi binafsi.
"Ni furaha yangu kuwa mafunzo yatatusaidia kuboresha ufanisi wa kazi kuendana na kasi ya maendeleo ya karne ya 21 na Dira ya Taifa 2050" amesema Mtulo".
Vilevile amewataka Mawakili wa serikali kushiriki kikamilifu mafunzo maalum yatakayotolewa ili kuwaandaa kutekeleza vema majukumu yao kuelekea uchaguzi mkuu ujao.
Post A Comment: