Mkuu wa Wilaya ya Ludewa Olivanus Thomas ametoa vyeti vya shukrani na pongezi kwa wananchi na wadau mbalimbali waliochangia kutokomeza upungufu wa madawati zaidi ya 3,000 kwa shule za Msingi na Sekondari ambapo mpaka sasa madawati 1,108 yamekwisha tengenezwa.
Akizungumza katika hafla hiyo mkuu huyo wa Wilaya amesema kuwa ushirikiano uliotolewa na jamii umewezesha wanafunzi wengi kupata mazingira bora ya kujifunzia, hivyo itasaidia kuimarisha ukuaji wa elimu katika wilaya hiyo.
Kwa upande wake, Afisa Elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi Bi. Munawara Swai, alieleza kuwa harambee hiyo iliyoanza Januari hadi Mei 2025, ilikusanya jumla ya Shilingi milioni 49.791,500 kutoka kwa wadau 89. Fedha hizo zilitumika kutengeneza madawati 1,108 kwa shule za sekondari, ambapo mbao 1,023 zilitumika katika utengenezaji huo.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa ndugu Castor Kibasa aliongeza kuwa mafanikio haya ni ushahidi wa mshikamano na uzalendo wa wananchi wa Ludewa katika kuhakikisha watoto wao wanapata elimu bora huku akisisitiza kuwa umoja huo ni chachu ya maendeleo endelevu katika wilaya hiyo.
"Harambee hii ni sehemu ya juhudi za serikali na jamii katika kuboresha sekta ya elimu na kuhakikisha kila mtoto anapata haki ya msingi ya elimu katika mazingira rafiki na salama."
Post A Comment: