Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje ya jiji la Dodoma maarufu kwa jina la Ring Road umefikia zaidi ya asilimia 85 ya utekelezaji wake.
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amepewa taarifa hiyo leo wakati alipokuwa akifanya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa mradi huo.
Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 112.3 ni miongoni mwa barabara za kimkakati mkoani Dodoma na katika ziara yake ya ukaguzi wa barabara hiyo jana, Ulega aliwaambia wana habari kwamba barabara hiyo itaung’arisha mji huo hasa nyakati za usiku kwani itafungwa taa za barabarani njia nzima.
“Nimekagua na nimeridhishwa na hatua zilizofikiwa katika awamu zote mbili na malengo ya Serikali ya Rais DKt. Samia Suluhu Hassan ni kuwa mradi huu ukamilike kwa wakati na nimeelekeza wataalam kutoka TANROADS hadi kufikia mwezi Juni ujenzi uwe umefikia asilimia 90”, amesisitiza Ulega.
Ulega alisema ujenzi wa barabara hiyo ni sehemu tu ya uboreshaji wa miundombinu ya barabara katika jiji la Dodoma na Tanzania kwa ujumla chini ya Rais Samia na waziri huyo ametumia ziara yake hiyo kutangaza kuwa serikali inatarajia kujenga barabara ya njia nne na sita kuanzia Chamwino Ikulu hadi katikati ya jiji hilo ambapo kwa sasa ipo katika hatua za mwisho za manunuzi za kumpata mkandarasi wa kujenga mradi huo.
Alisema katika eneo la Ihumwa, serikali ina mpango wa kujenga barabara ya kisasa ya njia za kupishana (interchange), ili kuruhusu magari kupita katika mji wa Serikali wa Magufuli na yaendayo mjini bila kuwa na kizuzi chochote.
Kwenye ziara yake hiyo, Ulega amesisitiza umuhimu wa taasisi za serikali,zikiwemo TANROADS, TRC na TPA kufanya kazi kwa kushirikiana ili kuwezesha mradi huo wa kimkakati kukamilika kwa wakati.
Kuhusu ujenzi wa miundiombinu ya ujenzi katika maeneo mengine, Ulega pia aliweka bayana kwamba ujenzi wa barabara za juu (flyovers) katika eneo la Morocco na Mwenge jijini Dar es salaam upo kwenye mpango mzuri na hatua iliyofikiwa sasa ni kuwa wizara inaendelea kukamilisha taratibu za kitaalam ili kuendelea na utekelezaji wa miradi hiyo.
“Nitumie fursa hii kuwaambia Watanzania kwamba bado Serikali inao mpango wa kuzijenga flyovers za Mwenge na Morocco na katika hatua iliyopo wataalamu wameniambia wanakamilisha taratibu na wafadhili wa mradi JICA hadi kufikia mwezi Julai fedha za mkopo zitakuwa zishasainiwa ”, amesisitiza Ulega.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa Barabara kutoka Wizara ya Ujenzi, Mhandisi Aloyce Matei amesema kuwa hadi kufikia mwezi wa saba matarajio yao ni kwamba fedha za mradi wa ujenzi wa barabara za juu za Morocco na Mwenge zitasainiwa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.
Naye, Mkurugenzi wa Miradi kutoka TANROADS, Mhandisi Japheson Nnko amemhakikishia Waziri Ulega kuwa watasimamia makandarasi hao kuhakikisha mradi wa mzunguko wa nje wa jiji la Dodoma unakamilika kwa ubora na wakati kama ilivyosainiwa kwenye mkataba.
Amebainisha kuwa mradi huo umegawanywa sehemu mbili ambapo mkandarasi China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) anayejenga sehemu ya Nala-Veyula-Mtumba-Ihumwa bandari kavu (km 52.3) anatarajiwa kukamilisha ifikapo mwezi Julai, 2025 na Mkandarasi Avic International anayejenga sehemu ya Ihumwa bandari kavu-Matumbulu-Nala (km 60) anatarajiwa kukamilisha ifikapo mwezi Agosti, 2025.
Post A Comment: