Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, ametoa wito kwa watumishi wa umma kuwa wabunifu katika kutafuta fursa za kiuchumi huku akiwatahadharisha dhidi ya maisha ya "maigizo" na utegemezi wa mikopo kutoka taasisi zenye masharti kandamizi.
Akizungumza Mei 1, 2025, katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), Mhe. Mtaka aliwataka watumishi kutumia muda wao wa kazi kugundua na kutumia fursa zilizopo katika maeneo yao ili kuongeza kipato halali nje ya mishahara yao ya kila mwezi.
“Acheni kuishi kwa ‘show off’. Tujifunze kujiwekea akiba, kuwekeza kwenye kilimo, biashara, na sekta ya misitu. Mnapokuwa kazini mkiona fursa, wekezeni. Msisubiri hadi mstaafu,” alisema Mtaka.
Akiendelea kuzungumza kwa Msisitizo jambo hilo Mhe. Mtaka alisema ni umuhimu kufanya maandalizi ya maisha ya baada ya ajira ambapo Mtaka alitaja wimbo wa ...msanii Alichoke uitwao Fainali Uzeeni... kuwa na ujumbe mzito kwa watumishi wa umma kuhusu umuhimu wa kupanga maisha mapema.
“Unapoomba kuongezewa mshahara ni kweli – lakini ukiongezewa, unautumiaje? Kuna watumishi wanakopa ili kufanyia matumizi yasiyo sahihi. Hii haipendezi,” aliongeza kwa kusisitiza.
Aidha, Mhe. Mtaka aliwapongeza watumishi wote waliotunukiwa zawadi za utumishi bora katika maadhimisho hayo, akiwahimiza kuendelea kujituma na kuwa mfano kwa wenzao katika utumishi wa umma.
Post A Comment: