Na Egidia Vedasto, Msumba News
Eneo la Stendi ndogo Jijini Arusha limekuwa katika mjadala wa muda mrefu, baada ya Baraza la Madiwani kuazimia kuboresha eneo hilo lenye kuwa wafanyabiashara takribani 400 kwa lengo la kuongeza mapato ya Jiji.
Akizungumza na Waandishi wa habari ofisini kwake Msitahiki wa Jiji la Arusha Maxmillian Iranqhe amesema serikali inawapenda wafanyabiashara na nia yake ni kuona wanafanya kazi katika mazingira yanayoridhisha na kukuza uchumi wao.
Aidha amebainisha kuwa lengo la kutaka kufanya maboresho katika eneo hilo, ni kutaka wafanyabiashara kufikia 2000 kutoka idadi ya sasa iliyopo ambayo ni wafanyabiashara 400.
Amesema kuwa sio busara kwa wafanyabiashara hao kuwa na mawazo hasi juu ya serikali, kwani kazi ya serikali ni kuhakikisha mapato yanaongezeka ikiendana na maboresho ya sehemu ya biashara.
"Hili ni azimio la Baraza la Madiwani, na lazima lifanyiwe kazi, hatuna nia mbaya bali tunataka kuona wafanyabiashara wakiongezeka ili kukuza mapato yetu" ameeleza Iranqhe.
Sambamba na hayo amewataka wananchi kuwa wavumilivu katika kipindi hiki cha mvua na baada ya hapo ukarabati wa barabara za ndani utaendelea kufanyika kama utaratibu ulivyowekwa hapo awali.
"Vifaa vipo kinachosubiriwa ni kipindi hiki cha mvua kupita ili kazi iendelee" amebainisha Iranqhe.
Mmoja wa wafanya biashara katika eneo la stendi ndogo (hakutaka jina litajwe) amesema suala la maboresho kama lilivyotajwa ni uonevu na nia ya kutaka kurudisha nyuma hatua zao za maendeleo.
"Sikubaliani na mambo ya maboresho, wakiamua wafanye wanavyotaka kwa sababu wana mamlaka, lakini kwa upande wangu hata wafanyabiashara wenzangu hatujawahi kuililia serikali kutuboreshea mazingira yetu ya kazi, kwa miaka yote hiyo tumekuwa tukifanya kazi zetu kwa utulivu lakini sasa naona wanataka kutuvuruga"amesema.
Post A Comment: