Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru (TICD), Dkt. Bakari George, amewaasa wataalamu wa Maendeleo ya Jamii Tanzania kuzingatia matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii katika utekelezaji wa majukumu yao.
Dkt. Bakari ameyasema hayo leo Mei 7, 2025, alipowasilisha mada inayoangazia tathmini ya awali ya Sera ya Maendeleo ya mwaka 1996 katika mkutano mkuu wa mwaka Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (CODEPATA) unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete (JKCC), jijini Dodoma.
Katika kusisitiza juu ya hoja hiyo, Dkt. Bakari huku akirejea takwimu zilizotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuwa watumiaji wa mitandao hapa nchini kuwa ni milioni 49.5, amesisitiza umuhimu wa wataalamu hao kuitumia mitandao hiyo kwa usahihi.
Katika hatua nyingine, Dkt. Bakari ameelezea malengo ya kuwasilisha tathmini hiyo katika kikao hicho kuwa ni kukusanya maoni kutoka kwa wataalam hao ambao ni ndiyo watekelezaji wakubwa wa sera hiyo.
Vile vile, Dkt. Bakari alifafanua hatua ambazo tathimini hiyo imepitia ikiwa ni pamoja na kuandika taarifa ya awali ya tathmini hiyo baada ya kukusanya maoni katika mikoa ya Dar es Salam na Dodoma kutoka kwa wadau mbalimbali kupitia kamati maalum iliyoundwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wnaawake na Makundi Maalum.
Mkutano huo wa Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii Tanzania ambao unafanyika kwa siku tatu (Mei 7 - 9, 2025) pamoja na mambo mengine, umelenga kuwakutanisha Wataalam wa Maendeleo ya Jamii Tanzania ili kujadiliana masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya Maendeleo ya Jamii Tanzania.
Post A Comment: