Na, Egidia Vedasto, Msumba News. 

Mkurugenzi wa elimu ya ufundi nchini Dkt. Fredrick Salukele ameridhishwa na kiwango cha ubunifu ulioonyeshwa na Wanafunzi wa chuo cha ufundi Arusha (ATC) katika maadhimisho ya wiki ya utafiti, ubunifu na ujasiriamali yaliyofanyika chuoni hapo. 

Akizungumza na wanafunzi hao walioshindanisha kazi za ubunifu 80 na kupatikana washindi 10 licha ya kutaja kuwa wote wamefanya vizuri, amewataka kufikiri zaidi juu ya kesho yao na kutamani kupiga hatua kubwa katika ubunifu ili waweze kukabiliana na soko la ajira duniani sambamba na kujiinua kiuchumi. 

Dkt. Salukele amesema,"Kiu yangu kwenu ni kuona mnakuza ubunifu huu na kuufanya uonekane Duniani kote, zipo taasisi nyingi zilianza kama nyinyi, lakini leo zimefanikiwa na kuwa mfano wa kuigwa na wengi, ongezeni bidii kila siku na kutangaza kazi zenu kupitia mitandao ya kijamii ili zijulikane, jicho la Dunia lipo kwenu mnaofanya elimu na ujuzi, mnategemewa kuhusu soko la ajira".

Hatahivyo amesema kuwa matokeo ya hatua hizi yametokana na nia njema ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alipotoa maelekezo kupitia upya sera ya elimu ya mwaka 2014 akitaka ujuzi kupewa kipaumbele katika sekta ya elimu. 

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo Prof. Mussa Chacha ameeleza kuwa wanafunzi hao wana upeo na uwezo mkubwa wa kubuni na kutafiti juu ya mambo mbalimbali. 

Pia ameomba ushirikiano wa karibu pale ikihitajika ili kwa pamoja waweze kufikia lengo la vijana kugueuza kazi  za ubunifu na kuwa pesa. 

Katika namna hiyohiyo Makamu mkuu wa chuo cha ufundi Arusha Dkt. Yusuph Mhando amesema dhumuni la wiki ya ubunifu ni kuhakikisha wanafunzi wote wanafanya mdahalo kuonyesha vipaji vyao, hatua itakayosaidia kuwanoa zaidi ili wagundue mapungufu na namna walivyopiga hatua. 

"Tutaendelea kuwasisitiza kuuza ubunifu wao ili kukabiliana na ukosefu wa ajira pamoja na kushirikiana na COSTEK kulea bunifu mbalimbali na kuziweka sokoni" amefafanua Dkt. Mhando.

Hanaan Mohamed msichana anayesoma elimu ya stashahada kozi ya uhandisi wa umeme na vifaa tiba katika chuo cha ATC, yeye na wenzake wametengeneza kifaa cha kuchunguza mishipa  (veinview) kitakachorahisisha kazi kwa watu wenye tatizo la kutoonekana mishipa kwa haraka na wale wanaotumia madawa ya kulevya. 

"Kwa ubunifu huu tunatarajia kufikia hospitali, vituo vya afya na zahanati hasa katika maeneo ya vijijini, sio kwamba kifaa hiki hakipo katika hospitali zetu, kipo lakini sisi tutakiuza kwa bei nafuu tofauti na bei ya kukinunua nje ya nchi, matarajio ni kuona kifaa hiki kinapatikana hadi kwenye zahanati za ndani kutokana na unafuu wa gharama zetu"ameeleza Hanaan. 

Vilevile Evodius Ngaiza anayesoma kozi ya Uhandisi wa ujenzi na barabara (stashahada) ameeleza kuwa, kazi zake za ubunifu zinaendana na teknolojia ya kisasa. 

"Mimi nafanya kazi ya kusanifu majengo na miradi ya kilimo cha umwagiliaji, matarajio yangu ni kuendana na kasi ya kidunia katika matumizi ya teknolojia ili  niweze kukabili soko la ajira" amesema Ngaiza.

Share To:

Post A Comment: