Mwenyekiti wa kamati ya uongozi ya Taifa ya TASAF Peter Ilomo ameipa mwezi mmoja kamati ya usimamizi miradi ya jamii TASAF kijiji cha Igomba kuhakikisha majengo ya zahanati ya kijiji hicho yanakamilika ili iweze kuanza kutoa huduma na kuwapunguzia adha wakazi wa Igomba kufuata huduma ya afya umbali mrefu.
Ilomo ametoa agizo hilo mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa majengo ya zahanati hiyo iliyopo katika kijiji cha Igomba wilaya ya Wanging'ombe mkoani Njombe ambapo amesema uwepo wa Zahanati ni muhimu katika kijiji hicho kwa kuwa wamekuwa wakifuata huduma ya afya kijiji jirani cha Isimike pamoja na kituo cha afya Saja vinavyopatikana umbali wa KM 6 kutoka kijijini hapo.
"Tujitahidi usiku na mchana,nimeambiwa mpango ni kumaliza mwezi wa tano lakini na mimi naongeza kidogo mpaka mwezi wa sita kwa kazi nilizoziona ili ikiwezekana mwezi wa saba huduma zianze kutolewa hapa"ameagiza Ilomo
Joyce Mdemwa ni Mratibu wa TASAF wilaya ya Wanging'ombe ameeleza kupokea maelekezo ya kukamilisha mradi huo huku wakazi wa Igomba wakishukuru kukamilishiwa zahanati yao ili kupunguza changamoto ya kufuata huduma ya afya umbali mrefu.
"Tunatarajia kukamilisha mradi huu tarehe theleathini mwezi wa tano na agizo la Mwenyekiti sisi tunamuahidi tutakamilisha na mwezi wa saba tutaanza kutoa huduma"amesema Joyce Mdemwa
Kijiji cha Igomba ni miongini mwa vijiji vya wilaya ya Wanging'ombe ambavyo vinanufaika na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ambapo licha ya kusaidia kaya maskini lakini pia kijiji hicho kilipokea Milioni 200.2 kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya Zahanati pamoja na nyumba ya mganga.
Post A Comment: