Na Benny Mwaipaja, New York


Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amesema kuwa Tanzania iko tayari kushirikiana na wadau mbalimbali zikiwemo serikali, mashirika ya kimataifa, sekta binafsi na asasi za kiraia ili kutafsiri kwa vitendo ahadi za Beijing+30 kuelekea Mkutano wa Nne wa Kimataifa kuhusu Ufadhili wa Maendeleo (FFD4), utakaofanyika kuanzia tarehe 30 Juni hadi 3 Julai 2025, Sevilla nchini Uhispania.

Dkt.Nchemba ameyasema hayo Jijini NewYork nchini Marekani, aliposhiriki mjadala ulioandaliwa na Taasisi ya Kimataifa inayojihusisha na masuala ya usawa wa kijinsia (UN Women), uliojikita kujadili namna ya kupata fedha kwa ajili ya kupunguza na kuondoa kabisa pengo la kijinsia katika uchumi na kuwawezesha wanawake kujikwamua kiuchumi wenye kauli mbiu isemayo “Kutoka Beijing hadi FfD4: Kuunganisha Ahadi Kupitia Ushirikiano wa Wadau kwa Usawa wa Kijinsia, Uwezeshaji wa Kiuchumi wa Wanawake na Maendeleo Endelevu”.

Alizitaja baadhi ya hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kuwawezesha wananwake na makundi mengine kiuchumi kuwa ni pamoja na kuwekeza katika elimu bora kwa wasichana hasa wa maeneo ya vijijini, kuwezesha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (WDF) na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana (YDF).

Dkt. Nchemba kuwa Serikali inatoa msaada wa kisheria bure kupitia kampeni kama Mama Samia Legal Aid Campaign ambayo hadi Februari 2025 ilikuwa imetoa msaada wa kisheria kwa wanawake 681,326.

“Tunatoa mafunzo ya elimu ya kifedha na ya kidijitali kwa wanawake na vijana kupitia huduma za uendelezaji wa biashara, tunatoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu na kukuza bajeti jumuishi kijinsia na kuhakikisha uchambuzi wa kijinsia unajumuishwa katika upangaji na utekelezaji wa bajeti ya umma” alisema Dkt. Nchemba.

Alisema kuwa pamoja na mafanikio hayo, bado kuna vikwazo vya kimfumo vinavyozuia wanawake kufikia uwezo wao kamili wa kiuchumi na kubainisha kuwa mchakato wa FfD4 ni fursa muhimu ya kuhakikisha upatikanaji wa rasilimali za kifedha, sera jumuishi, na ushirikiano wa kibunifu unaoipa kipaumbele usawa wa kijinsia, kwa ajili ya kasi zaidi ya maendeleo.

“Tanzania inaipongeza UN Women kwa kuandaa nyaraka ya rasilimali (resource paper) inayotoa mwongozo wa kisera wa kifedha kwa mtazamo wa kijinsia. ambayo ni nyenzo muhimu  itakayosaidia kuhakikisha kuwa uwezeshaji wa kiuchumi wa wanawake unakuwa kiini cha majadiliano na matokeo ya FfD4”. Aliongeza Dkt. Nchemba

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Sera, Programu, Divisheni ya ushirikiano wa Kimataifa wa UN Women, Bi. Sarah Hendriks, alisema kuwa suala la kuwawezesha wanawake kiuchumi linapaswa kuwa agenda ya kudumu ya mataifa mbalimbali hususan ya kiafrika ili kujenga jamii yenye nguvu ya kiuchumi kupitia uwekezaji wa mitaji, elimu, biashara na kuwawezesha kufikia masoko kwa njia ya kidigiti.

Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban na uliwashirikisha wadau kutoka sekta mbalimbali

Share To:

Post A Comment: