Viongozi wa serikali za mitaa wameapishwa tarehe 29, Novemba 2024, huku Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala Bi. Rose Manumba akishiriki zoezi hilo ambapo amewataka Wenyeviti wa Vijiji, Vitongoji na Wajumbe wa Serikali za Vijiji kusimamia vyema maendeleo na kutatua changamoto zinazojitokeza na kutokuwa chanzo cha migogoro na kulinda amani, ulinzi na usalama katika maeneo yao kwa mujibu wa sheria kwa kuzingatia usawa.
Bi Rose Manumba ameyasema hayo leo wakati wa zoezi la kuapishwa kwa Viongozi na Wajumbe wa Vijiji na Vitongoji katika halmashauri hiyo, ambapo amesema kwa sasa uchaguzi umekwisha na kwamba wanapaswa kuongea lugha moja ili kuwaletea wananchi maendeleo katika maeneo yao.
Aidha, Manumba amewataka wakasimamie maadili kwa jamii kwa kupiga vita vitendo na mienendo itakayokiuka mila, tamaduni, desturi na sheria za nchi pamoja na kutoa taarifa kwa wananchi mara kwa mara.
Katika hatua nyingine, amesema kuwa wanapaswa kuzisikiliza na kuzitatua changamoto za wananchi, zinazowashinda ziwasilishwe kwa wakati ngazi za juu za utawala kwa utatuzi zaidi.
Jumla ya wenyeviti wa Vijiji 92, Wenyeviti wa Vitongoji 389 na Wajumbe wa Serikali za Vijiji 1821 wameapishwa leo na kuanza majukumu yao kwa kuzingatia taratibu, Sheria na kanuni za Nchi.
Post A Comment: