SERIKALI imetenga kiasi cha shilingi Bilioni 1.4 kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETTA) wilayani Muheza Ili kuwapa nafasi vijana kujifunza stadi za maisha.

Akizungumza katika mkutano wa elimu wilayani Muheza, Mbunge wa Muheza ambaye pia ni Naibu Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe Hamisi Mwinjuma almaarufu MwanaFA, alisema tayari chuo hicho kimeanza kujengwa katika kata ya Kilulu baada ya serikali kutoa kiasi cha shilingi milioni 300 za awali.

Akizungumza katika mkutano huo uliokuwa na zaidi ya walimu 2,000 alisema kupatikana chuo hicho ni jitihada alizofanya kuiomba serikali ilete fedha kukamilisha mradi huo Ili kutoa fursa kwa vijana kujifunza fani mbalimbali.

"Nikushukuru mhe Waziri (Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teklonojia mhe Omari Juma Kipanga) wakati wetu wa kupata chuo hiki ulikuwa bado lakini nilikuomba kutokana na mahitaji yetu, nashukuru mmetuletea fedha za awali shilingi milioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa cheo chetu," alisema MwanaFA.

Mbunge huyo wa Muheza ambaye ni kipenzi cha watu, alitumia fursa hiyo kutuma salamu kwa Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa jinsi miaka mitatu ya uongozi wake ameweza kuwatendea haki wananchi wa Muheza kwa kuleta fedha kiasi cha shilingi Bilioni 8.4 ambazo zimejenga miundombinu ya shule wilaya humo.

"Mheshimiwa Waziri tunatuma shukrani kwa mhe Rais kwa suala la elimu, hatuna posta nyingine isipokuwa wewe unayemwakilisha serikali katika Wizara ya Elimu utufikishie salamu zetu za shukrani kwake kwakweli ametutendea haki na tunashukuru," alisema na kuongeza,

"Juzi nilikuwa tarafa ya Amani diwani mmoja wa kata ya Kisiwani alisema haijawahi kutokea kwa kipindi cha miaka 16 katika kata yao ilipokea shilingi 12 lakini sasa Kwa miaka hii mitatu kata yake imepokea kiasi cha shilingi Bilioni 2.6 katika elimu,".

MwanaFA alisema kutokana na kasi ya kujenga shule mipango yao kwa sasa ni kuhakikisha wanaongeza shule za elimu ya juu (High school) kutoka mbili zilizopo sasa hadi kufikia shule Sita.

Alizitaja shule ambazo wanampango wa kuzifanya ziwe shule za elimu ya juu kuwa ni Kwabastola, Kilulu, Kicheba na Ngomeni. Hivi sasa zilizopo ni Muheza na Songa.

"Utaona kabisa kwa jitihada hizi Muheza inarudi historia yake kuwa sehemu ya maeneo bora yanayotoa elimu na eneo bora inayotoa wasomi bora katika nchi hii," alisema MwanaFA.

Awali Mkuu wa wilaya ya Muheza Zainab Abdallah alimpongeza mbunge Kwa kufanikisha mkutano huo ambao umefungua fursa ya kuhakikisha wanasimamia elimu Ili watoto waweze kusoma na kufaulu vizuri.

Mgeni rasmi katika mkutano huo Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teklonojia mhe Omari alisema serikali inawapongeza walimu nchini kwa kazi nzuri ya kuendelea, kuwalea na kuwafundisha kimaadili na kitaaluma licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali.

Alisema Rais Dkt Samia Suluhu Hassan anatambua mchango wa walimu nchini pamoja na changamoto lakini ufaulu kwa wanafunzi umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka.

Alisema serikali inafanya juhudi za uboreshwaji wa mazingira ya kufundishia ikiwemo ujenzi wa nyumba za walimu, madarasa, mabweni pamoja na kuboresha stahili za walimu na upandishwaji wa madaraka.

Pia alisema tayari ajira za walimu wapya 12,000 zimetangazwa na kwamba serikali imehuisha sera ya Elimu na mafunzo ya Ufundi ya mwaka 2004 hadi 2024.

Alisema uboreshwaji huo ambao pia umehusisha mitaalam mipya ya shule za msingi na vyuo vya elimu Ili kuendana na soko la sasa la ajira na baadae.

"Sera mpya toleo 2023 umelenga katika msingi mkubwa wa kufundisha wanafunzi wajikite katika malengo, maadili, umahiri, ujuzi ambao utamwezesha kijana akimaliza elimu yake aweze kujiajiri," alisema.


Share To:

Post A Comment: