Watumishi wa Tume ya Utumishi wa Umma kesho jumamosi Septemba 28, 2024 watakwenda kutoa msaada wa kibinadamu kwa wazee wa Kituo cha Samaria Hombolo wanaokabiliwa na changamoto ya ugonjwa wa ukoma na macho, ikiwa ni pamoja na kupanda miti Mtumba katika jengo jipya la ofisi yao kwa lengo la kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Hayo yamesemwa na Katibu wa Tume hiyo ya Utumishi wa Umma Bw. Methew Kirama, wakati akieleza namna Siku ya Tume (Tume Day) itakavyoadhimishwa kesho kwa kutunza mazingira na kufanya matendo ya huruma kwa wenye uhitaji maalum Hombolo.
Akizungumzia zoezi la upandaji miti kabla ya kwenda Hombolo kwa wenye uhitaji, Bw. Kirama amesema upandaji miti katika jengo la ofisi ya tume linaloendelea kujengwa katika Mji wa Serikali Mtumba, utaongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Utumishi na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene akiambatana na Makamishna wa Tume pamoja na watumishi.
Bw. Kirama amesema, mara baada ya zoezi la upandaji miti kukamilika, watumishi wa Tume ya Utumishi wa Umma na Makamishna wataelekea Hombolo kutoa msaada wa kibinadamu kwa wazee wenye uhitaji wa Kituo cha Samaria.
“Tume imejenga vyoo 8 ambavyo tutavikabidhi kesho lakini pia tutapeleka vyakula, nguo, mafuta na mahitaji mengine muhimu ili nao wajione ni wanajamii wenzetu na wanathaminiwa,” Bw. Kirama amesisitiza.
Bw. Kirama amefafanua kuwa, watumishi wa Tume ya Utumishi wa Umma wamejitoa na kufanikiwa kupata nguo, vyakula na mafuta kwa ajili ya kuwapelekea wenye uhitaji Hombolo, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais ambaye amekuwa mstari wa mbele kutoa msaada wa kibinadamu kwa makundi yenye uhitaji nchini.
Kwa upande wake, Katibu wa TUGHE tawi la Tume ya Utumishi wa Umma Bw. Gift Lyimo amesema kuwa amewahamasisha watumishi wenzie kuungana ili kufanikisha lengo la ofisi la kupeleka vyakula, maji, mavazi na kukabidhi vyoo 8 na kuongeza kuwa kitendo hicho kitakuwa ni faraja kwa wenye uhitaji katika Kituo hicho cha Wazee wa Samaria Hombolo.
Naye, Afisa Utumishi Mkuu wa Tume ya Utumishi wa Umma Bi. Neema Mkenda amesema, kitendo cha watumishi wa Tume ya Utumishi wa Umma kuamua kwenda kutoa msaada wa kibinadamu kwa wenye uhitaji Hombolo ni ishara ya kuunga mkono kwa vitendo juhudi za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuwasaidia wenye uhitaji nchini.
Tume ya Utumishi wa Umma imeona ni vyema kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu kwa kupanda miti ili kuifadhi mazingira na kufanya matendo ya huruma kwa wenye uhitaji Hombolo kama ambavyo Mhe. Rais amekuwa akifanya na kusisitiza kila mmoja kwa nafasi yake afanye matendo hayo ya huruma.
Post A Comment: