Na. Joseph Mahumi, WF, Dar es Salaam


Wananchi wamekumbushwa kuendelea kuwaruhusu Watoto wao kujifunza Elimu ya Mikopo hasa kwa vijana wa umri wa chini na pia wao kama wazazi kuchangamkia fursa zilizopo katika vyama vya kuweka na kukopa fedha (SACCOSS) ikiwemo HAZINA SACCOSS, kwa kuwa vyama hivyo vimekuwa ni suluhisho la mikopo chechefu kwa kutoa riba nafuu ikilinganishwa na taasisi nyingine za fedha.

Hayo yamesemwa na Mtendaji Mkuu wa Hazina SACCOSS, Bw. Festo Mwaipaja, wakati wa Mashindano ya Hazina Club ambayo yameratibiwa na HAZINA SACCOSS na kuwakutanisha wanafunzi kutoka Shule za Sekondari za Kisutu, Kigogo, Turiani, Mzimuni, Migombani, Minazi Mirefu, Tambaza, Makumbusho, Kambangwa na Kinyerezi, za mkoani Dar es Salaam, ambapo wameshindania masuala mbalimbali yanayohusu masuala ya Elimu ya Fedha, Mikopo inayotolewa na HAZINA SACCOSS na fursa zilizopo katika vyama vya ushirika.

Bw. Mwaipaja alisema kuwa, Mashindano hayo yamelenga kuwaanda vijana mashuleni kuwa na ufahamu wa namna ya kusimamia fedha ili kuleta tija pale ambapo wataanza kujitegemea ili wawe na nidhamu nzuri ya kusimamia fedha zao.

“Mafunzo tunayotoa hapa yatawasaidia watoto na taifa kwa ujumla kwa kuwa watawaelimisha pia wazazi wao na jamii iliowazunguka, na tutakua tumefikisha elimu kwa watanzania wengi” alisema Bw. Mwaipaja.

Bw. Mwaipaja aliongeza kuwa, Changamoto ya elimu ya fedha ni kubwa duniani na endapo tukifanikiwa kupambana na changamoto hiyo ni dhahiri itafanikisha kupambana na umasikini.

Aliongeza kuwa, kwa ujumla wanafunzi waliofika katika mashindano hayo, wamepata elimu kubwa sana na itaongeza chachu ya elimu ya fedha kusambaa zaidi, mashuleni, majumbani na manufaa ya program hiyo yatakuwa makubwa katika siku za usoni.

“Nawasihi watumishi wa umma kujiunga na HAZINA SACCOSS, kwa kuwa itawasaidia kupata mikopo ya riba ndogo sana ambayo itawasaidia hususan katika kipindi ambacho wanafunzi wanafungua shule au pale wanapopata changamoto au dharura maarufu kama “Tuliza Moyo”, na sisi tupo hapa kuwasaidia kwa kuwa ni mahali sahihi kwa watumishi” aliongeza Bw. Mwaipaja.

Kwa upande wake Mwalimu wa Shule ya Misingi Kigogo, Bw. Florence Mafaransa, ambaye ameshiriki pamoja na Wanafunzi wake katika Mashindano hayo, alisema kuwa mashindano hayo ni muhimu kwa vijana wa taifa la kesho kwa kuwa yatawawezesha kujua namna ya kujipanga na maisha yao.

“Tunaishauri Serikali iendelee kutoa mafunzo kama haya kwa vijana mashuleni ili kuandaa taifa la kesho kuweza kusimamia fedha na kupata wananchi wanaokopa katika vyanzo sahihi vilivyo rasimishwa na Serikali” alisema Bw. Mafaransa

Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi walioshiriki mashindano hayo, Paul Mwita Sibora kutoka Shule ya Sekondari Tambaza, aliishukuru HAZINA SACCOSS kwa kuanza kutoa elimu ya fedha kuanzia ngazi ya chini kabisa kwa kuwa ni njia bora ya taifa la kesho.

“tutakua mabalozi bora kwa wazazi wetu na watu waliotuzunguka na kuwaeleza namna ya kujiunga na pia fursa zilizopo Hazina Saccoss“ alisema Bw. Sibora.

Mashindano hayo yanatarajiwa kuendelea nchi nzima kupitia Shule za Sekondari ikiwa na lengo kubwa la kuhakikisha vijana wa taifa la kesho wanakua na uwezo wa kusimamia vyema masuala ya fedha.
Share To:

Post A Comment: