Watumishi Housing Investments (WHI) inatarajia kutekeleza mradi wa nyumba 101 katika eneo la Mikocheni Regent Estate jijini Dar es-salaam.
Ujenzi huo utaanza Mwezi Agosti 2024 na unahusu ujenzi wa jengo la ghorofa 12 lenye nyumba 101 ambapo kila mnunuzi atamilikishwa nyumba atakayoinunua ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Makazi kwa Watumishi wa Umma (Public Servant Housing Scheme) unaotekelezwa na WHI.
WHI tayari imejenga nyumba 1,003 katika mikoa 19 nchini Tanzania na nyumba 101 ambazo utiaji Saini na Mkandarasi Shadong Hi-Speed Group umefanyika leo tarehe 30 Julai 2024, ni sehemu ya nyumba 218 zitakazojengwa katika mikoa ya Dodoma, Lindi, Mtwara, Singida, Pwani na Ruvuma katika mwaka wa fedha 2024/2025.
Ujenzi wa mradi huu wa nyumba 101 utagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 18.6 na ujenzi wake utafanyika kwa kipindi cha miezi 18. Nyumba hizi zitauzwa kwa utaratibu maalum wa unafuu kwa watumishi wa umma. Bei ya nyumba ya chumba kimoja yenye sebule, chumba cha kulala, choo, stoo, jiko, balcony n.k., itaanzia Shilingi Milioni 99 na bei ya nyumba ya vyumba vitatu vya kulala, sebule, stoo, balcony n.k itaanzia Shilingi Milioni 234/=. Bei za nyumba hizi zikilinganisha na nyumba za aina hii katika eneo la Mikocheni, nyumba hizi ni nafuu kwa kati ya asilimia 10% hadi 40%. Uuzaji wa nyumba hizo tayari umeanza, na tunatarajia mwitikio mkubwa kutoka kwa walengwa. Huu ni mradi unaolenga kuwapa watumishi wa umma fursa bora za umiliki wa makazi yenye thamani na ubora.
Watumishi Housing Investment ni taasisi ya umma chini ya Ofisi ya Rais UTUMISHI yenye jukumu la uendelezaji wa milki na usimamizi wa uwekezaji kupitia uanzishaji na usimamizi wa mifuko ya uwekezaji wa Pamoja. WHI inasimamia mifuko miwili yaani Mfuko wa Nyumba Pamoja na mfuko wa Faida Fund.
Post A Comment: