Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameeleza kuwa kiasi cha Shilingi Bilioni 34 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha pamoja cha Forodha  (One Stop Boarder Post- OSBP) katika eneo la Manyovu ambapo ni mpaka wa nchi ya Tanzania na Burundi ili kuwezesha Mkoa wa Kigoma kufanya biashara na nchi jirani.

Bashungwa ameeleza hayo wakati akizungumza na wananchi wa Mnanira, Manyovu katika ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ya kukagua miradi ya maendeleo mkoani Kigoma.

“Wizara ya Ujenzi tayari tupo katika hatua ya kumtafuta Mkandarasi wa kujenga kituo cha kisasa ndani ya nchi yetu ya Tanzania, bilioni 34 zimeshatengwa kwa ajili ya kuanza ujenzi huo”, ameeleza Bashungwa.

Bashungwa amefafanua kuwa Kituo hicho kitakuwa cha kisasa na kikikamilika kitasaida kuboresha biashara na kuwezesha Mkoa wa Kigoma kuwa kitovu cha biashara kwa nchi yetu na nchi za jirani za Burundi na DRC Congo.

Aidha, Bashungwa ameeleza kuwa Wizara ya Ujenzi itashirikiana na Wizara ya Fedha kuhakikisha wanawalipa fidia wananchi watakaopisha ujenzi wa Kituo cha Pamoja cha Forodha kiasi cha Shilingi Bilioni 1.7 kabla ya kuanza ujenzi wa kituo hicho.

Katika hatua nyingine, Bashungwa ameahidi kuwakabidhi wananchi wa Mkoa wa Kigoma barabara ya Malagarasi – Ilunde – Uvinza (km 51.1), Kasulu - Buhigwe hadi Manyovu (km 68.2) na barabara ya Kasulu – Kibondo (km 16) zilizobakia kujengwa kwa kiwango cha lami ifikapo mwezi Machi, 2025 ili kurahisisha shughuli za kibiashara na uwekezaji katika Mkoa huo.

Vilevile, Bashungwa ameeleza katika mradi wa barabara ya Kasulu - Buhigwe - Manyovu Wakala ya Barabara (TANROADS) watajenga barabara ya mzunguko ya kisasa (roundabout) katika mji wa Buhigwe ili kuupendezesha mji huo.

Akitoa taarifa ya mradi, Meneja wa Wakala ya Barabara (TANROADS) Mkoa wa Kigoma Mhandisi Narcis Choma amebainisha miradi ya kusaidia jamii (CSR) iliyopo katika mradi wa barabara ya Kasulu - Buhigwe – Manyovu ambapo kwa Wilaya ya Buhigwe watajenga miundombinu ya maji safi na maji taka, ujenzi wa Kituo cha Mabasi pamoja na ukarabati wa Soko la Buhigwe na kueleza kuwa Wakandarasi wa kazi hizo tayari wameshapatikana wapo tayari kuanza kazi muda wowote.

Share To:

Post A Comment: