Elizabeth Joseph,Arusha.

Jamii nchini imeshauriwa kuacha kutumia neno Chizi,Dishi limeyumba na Kichaa katika majukwaa mbalimbali kwakuwa kutumia maneno hayo ni kuzidi kuonesha hali ya unyanyapaa kwa wenye tatizo la afya ya akili.

Ushauri huo umetolewa Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe Dkt,Paul Lawala wakati wa kikao cha waandishi mbalimbali wa Habari nchini pamoja na wataalam wa masuala ya Afya ya Akili kilicholenga kujadili juu ya Afya ya Akili kwa ujumla.

Dkt Lawala amesema kuwa hakuna ufahari wa kutumia maneno hayo kama utani ama kuashiria ujumbe fulani kwani kufanya hivyo ni kurudisha nyuma jitihada za serikali katika kupinga unyanyapaa katika afya ya akili nchini.

"Kutamka maneno ya kinyanyapaa yaliyozoeleka kama Chizi,Una file Mirembe,Kichaa hasa katika majukwaa ya dini na siasa tuache kwakuwa sio ufahari na hatupaswi kuchukulia mzaha katika hili "amefafanua Dkt Lawala.

Aidha amewataka Waandishi wa Habari kubadilika katika kuripoti habari zinazohusu afya ya akili kwa kuepuka kutumia majina hayo katika habari zao ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanakuwa na ushahidi wa kisayansi kabla ya kuripoti habari zao zinazohusu masuala hayo.

Kwa upande wake Dkt Godwin Mwisomba ambaye ni Daktari Bingwa wa Afya ya Akili ameitaka jamii kuacha imani na mila potofu kwakuwa vitendo hivyo vinarudisha nyuma jitihada katika kuondokana na tatizo hilo.

"Zaidi ya asilimia 65 ya wagonjwa wanaokuja kutibiwa wanakuwa washapita kwenye Imani za kitamaduni kabla ya kuja Hospitali, watu wamekuwa na mila potofu kwa kuamini ndugu yao amelogwa wakati ukimuangalia unajua shida ni nini hivyo jamii bado inahitaji kuelimika kwa kuachana na hizi mila ili kuwatibu watu hawa kwa wakati"Amesema Dkt, Mwisomba.

Pia ameitaka jamii kutojinyanyapaa pindi wanapopatwa na changamoto ya afya ya akili na hivyo kutafuta wataalam wa masuala hayo ili kupata tiba sahihi kwakuwa tiba nyingine zinahusu maongezi pekee na sio matumizi ya dawa.

"Mtu anakaa na tatizo na kushindwa kusema kwa kuhofia jamii itamchukuliaje hivyo anaanza kujinyanyapaa mwenyewe lakini ingekuwa wanajikubali na kuwa huru kushare matatizo yao ingesaidia kwa kiasi kikubwa kutatua tatizo lao"Ameongeza kusema Dkt,Mwisomba.

Share To:

Post A Comment: