Na Mapuli Kitina Misalaba

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi  Macha ametoa wito kwa wananchi Mkoani Shinyanga kuwa na utamaduni wa kupima Afya ili kufahamu hali ya Afya na namna ya kujilinda na magonjwa mbalimbali ikiwemo magonjwa ya kuambukiza.

Ameyasema hayo leo Jumanne Juni 18,2024 wakati  akizungumza na wananchi waliojitokeza kupata huduma bure  ya Macho pamoja na huduma zinazotolewa na madaktari  bingwa wa Rais Samia katika Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga.

RC Macha amesisitiza wananchi kujitokeza katika huduma hizo huku akihimiza kuwa na utaratibu wa kupima Afya mara kwa mara badala ya kusubiri kupatwa na ugonjwa.

“Ni vizuri wananchi kujenga utamaduni wa kupima Afya zao wagonjwa wengi ambao wanakuja Hospitali ni wagonjwa ambao pengine magonjwa yao yangeweza kuwa yametibika au yameisha kabisa kama wangewahi kuja kupima yapo magonjwa kama Saratani kwa upande wa akna Baba kuna matatizo ya tezi dume, kuna matatizo ya figo, kuna matatizo ya mafuta kwenye miili yetu, kuna tatizo la Sukari haya yote ni magonjwa ambayo kama tungeliweza kuwahi mapema katika Hospitali tukafanya vipimo mfano ugonjwa wa Saratani ukiwahi mapema ukifahamika uvimbe uvimbe kwenye maeneo yetu ya mwili ule ugonjwa unaisha kabisa, tumekubaliana na nitakaa na viongozi wangu mganga mkuu na mamlaka zingine zote za Afya katika Mkoa tutenge siku mbili kwa Mwezi ziwe ni mahususi kwa ajili ya watu kupima Afya zao”.amesema RC Macha

Pia Mhe. Macha baada ya kutembelea ukarabati wa majengo katika Hospitali hiyo amempongeza mganga mkuu wa Manispaa ya Shinyanga kwa usimamizi mzuri katika ujenzi na ukarabati wa majengo hayo.

“Lazima niseme ukweli kwa sababu kuna nyakati tunafika mahali tunakemea kemea watendaji lakini mali pengine ukifika ukawakuta watendaji wanafanya kazi vizuri unawasifu kwakweli ni lazima tumsifu sana DMO wa hapa kazi anayoifanya kwa hakika niyakuridhisha na tunaposema DMO lazima tuwashukuru na watumishi wa hapa kwa kazi wanazofanya tunaona n kazi nzuri na tunazidi kuwatia moyo kuwahudumia wagonjwa ni kazi kubwa sana kwahiyo inahitaji zaidi kwa wakati mwingine hata na utume zaidi ya utumishi”.amesema RC Macha

Kwa upande wake mganga mkuu wa Manispaa ya Shinyanga Dkt. Elisha Robert  ameeleza hatua zilizofikiwa katika ukarabati na ujenzi wa majengo ya kutolea huduma ambapo amesema ujenzi na ukarabati wa majengo hayo unagarimu zaidi ya bilioni moja.

“Tunatarajia ifikapo Juni 30 ukarabati wa jengo la upasuaji utakuwa umekamilika pia zile wodi mbili za wanaume na wanawake nazo zitakuwa zimekamilika lakini tunafanya pia ukarabati wa jengo la kutunzia dawa tunaimani pia ifikapo tarehe 30 Mwezi huu itakuwa imekamilika, maboresho yote ambayo tunayafanya ndani ya Hospitali hii ya Manispaa ya Shinyanga ambayo yanajumuisha ujenzi pamoja na ukarabati wa miundombinu ikiwemo ujenzi wa jengo la dharura, ujenzi wa jengo la OPD, ukarabati wa jengo la upasuaji, wodi mbili za wazazi, jengo la kutunzia dawa, jengo la mionzi pamoja na ukarabati mdogo wa jengo la maabara, CTC na TB clinic utagharibu shilingi bilioni 1.3 fedha hizi tumeshazipokea kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan”.amesema Dkt. Elisha

Katika taarifa ya uboreshaji miundombinu ya Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga iliyosomwa na kaimu Daktari mfawidhi Dkt. Moshi Lyoba pamoja na mambo mengine amesema Hospitali hiyo inachangamoto ya upungufu wa watumishi, vifaa tiba pamoja na uchakavu wa miundombinu.

“Manispaa ya Shinyanga ilipokea huduma za Afya zilizokuwa zinatolewa na Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Shinyanga hii ni kufuatia kukamilika kwa ujenzi wa Hospitali mpya ya rufaa ya Mkoa wa Shinyanga iliyopo katika kata ya Mwawaza ambayo tayari imeshaanza kutoa huduma za Afya upokeaji wa huduma za Afya kwenye Hospitali hii ulifanyika kuanzia tarehe 01.07.2023”.

“Huduma zinazoendelea kutolewa ndani ya Hospitali baaada ya kupokea ni huduma za wagonjwa wan je (OPD), huduma za dharura (EMD), huduma za uzazi kwa Mama wajawazito ikiwemo na upasuaji, huduma ya kulaza watoto, wanaume na wanawake, huduma za kulaza watoto wachanga (NICU), huduma za maabara, huduma za mionzi (X-ray na Ultrasound), huduma za tiba na matunzo (CTC), huduma za kifua kikuu, huduma za kuhifadhi maiti, huduma za kinywa na meno na huduma kwa wagonjwa wa bima (NHIF na Ichf)”.amesema Dkt. Lyoba

 “Manispaa ya Shinyanga ilipokea fedha kiasi cha shilingi 1, 300, 000,000\= kwa awamu mbili tofauti kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ambapo awamu ya kwanza kiasi cha shilingi 500, 000,000\=  kilipokelewa tarehe 04.01.2024 na kufuatiwa na mapokezi ya shilingi 800,000,000\= katika awamu ya pili, kiasi hiki cha fedha kilipokelewa kwenye akaunti ya Hospitali tarehe 26.02.2024 fedha hizi zimelenga kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma za Afya kwa kujenga jengo la dharura, jengo jimpya la wagonjwa wa nje na njia za waenda kwa miguu (walk way), kufanya ukarabati wa jengo la upasuaji, wodi mbili za upasuaji, jengo la kutunzia dawa na jengo la mionzi pia kufanya ukarabati mdogo wa jengo la ICU, Maabara, CTC na TB clinic”.

“Lengo la mradi ni kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma za Afya kwa wakazi 214, 744 wa Manispaa ya Shinyanga na maeneo jirani, mradi huu wa uboreshaji wa miundombinu ya kutolea huduma za Afya ndani ya Hospitali unatarajia kukamilika ifikapo Juni 30, 2024”.

“Hadi kufikia tarehe 18,06,2024 ujenzi na ukarabati huu ulikuwa umegharimu kiasi cha shilingi 1,023,543,500\=  hii ikiwa ni gharama za vifaa vya ujenzi na ufundi ambazo zimelipwa kiasi cha shilingi 276,456,500 hazijatumika aidha vigae kwa ajili ya jengo la OPD vimenunuliwa toka kiwandani”.amesema Dkt. Lyoba

Wakizungumza na Misalaba Media baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Shinyanga wametoa shukurani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kupitia serikali yake ya awamu ya sita kwa kuamua kuboresha mazingira ya kutolea huduma za Afya hali ambayo itasaidia kuendelea kuimarisha Afya za wananchi.

Wananchi hao ambao wamepata huduma mbalimbali ikiwemo huduma ya Macho wametumia nafasi hiyo kuipongeza serikali kwa kuanzisha utaratibu huo huku wakiomba kuwa endelevu ili kupunguza au kumaliza kabisa changamoto za kiafya.Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha katika ziara yake ameongozana na viongozi mbalimbali wa serikali pamoja na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi CCM.

Mganga mkuu wa Manispaa ya Shinyanga Dkt. Elisha Robert  akizungumza leo Juni 18,2024.

Mganga mkuu wa Manispaa ya Shinyanga Dkt. Elisha Robert  akizungumza leo Juni 18,2024.


 

Share To:

Misalaba

Post A Comment: