Na. John I. Bera - Arusha
Watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii wamepongezwa kwa kuwa ni miongoni mwa wanamichezo, walioshiriki Mashindano ya Mei Mosi kwa mwaka 2024 ambapo zaidi ya washiriki 2000 kutoka wizara na taasisi wameshiriki katika mashindano hayo kwa mwaka huu Jijini Arusha
Akizungumza wakati akifunga mashindano hayo leo Aprili 29, 2024, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Bw. Tumaini Nyamhokye amesema nifaraja kuwaona watumishi hao wanaendelea kushiriki mashindano hayo kila mwaka huku akisisitiza kuwa kwa kufanya hivyo wanaimarisha utendaji kazini kwa kuwa na afya njema
"Nichukue fursa hii kuzipongeza Timu zote zilizoshiriki mashindano haya kwa mwaka huu, tulikuwa na timu 56 kutoka Wizara pamoja na Taasisi, jambo hili ni kubwa sana kwetu, natumaini mashindano haya yataweza kuimarisha afya za watumishi hawa " Amesema Nyamhokyea
Aidha, amesema wao kama Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) watahakikisha wanahamasisha michezo hiyo kila mwaka ili kuendeleza utamaduni wa kuhakikisha wanaimarisha afya za wafanyakazi na ushrikiano kupitia michezo
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Michezo Mei Mosi Taifa, Bi. Roselyne Massam , ameushukuru uongozi wa Mkoa wa Arusha kwa ushirikiano na hatimaye kufanikisha mashindano hayo ambayo yamefanikiwa kufanyika na kutamatika salama
Vilevile, amewashukuru viongozi wa Wizara pamoja na Taasisi za Serikali kwa ajili ya kuwaruhusu watumishi wao kushiriki michezo hiyo huku akisisitiza kuwa ushiriki wao unaimarisha afya zao, lakini pia unaleta ushirikiano wa pamoja baina ya watumishi na kujenga umoja unaosaodia katika utendaji kazi
Katika Mashindando hayo ambayo yametamatika leo, Wizara ya Maliasili na Utalii imefanikiwa kushinda vikombe viwili ambapo ilipata kikombe kimoja kwa kumaliza mshindi wa tatu kwenye mchezo wa Drafti na kikombe kimoja kwa kumaliza mshindi wa tatu wa jumla kwenye mchezo wa Riadha (Overall 3rd Winner) huku ikipata medali tano ambapo nne zilipatikana kwenye Riadha kwa kushinda mshindi wa tatu kwenye mbio za mita 3000, 1500 , 800 na 200 huku medali moja ikipatikana kutoka kwenye mchezo wa kurusha Tufe.
Post A Comment: