Atatua mgogoro wa wamachinga na Mama Lishe kuhamishwa


Ashauri wasiondolewe katika maeneo yao kwa sasa


Ampongeza Mkurugenzi Kayombo kwa utatuzi wa changamoto kwa haraka


Awaasa wafanyabiashara wadogo kufuata utaratibu 


Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Anthony Mavunde ameahidi kuwaboreshea mazingira ya utoaji huduma Mama Lishe wa Stendi Kuu Dodoma kwa kuwapatia meza nadhifu na vifaa vya kisasa vya kutolea huduma ya Chakula.

Mh Mavunde ameyasema hayo leo wakati wa mkutano wa wafanyabiashara wadogo,Mama Lishe na uongozi wa Halmashauri ya  Jiji la Dodoma kwa lengo la kutatua changamoto ya uhamishwaji wa wafanyabiashara hao katika maeneo ya stendi kuu Jijini Dodoma.

“Madhumuni ya ujenzi wa stendi hii ni kutoa huduma ya usafirishaji na pia kuchochea uchumi wa wananchi wa Dodoma kupitia biashara mbalimbali.

Nishauri uongozi wa Jiji kuwapangia utaratibu mzuri wafanyabiashara hawa wafanye biashara hii kwa muda na baadaye watarejea katika maeneo rasmi baada ya mzunguko wa biashara kuimarika sokoni hapa.

Nitawasaidia Mama Lishe meza nadhifu na vifaa vya kisasa vya kutolea huduma ili msichafue mazingira hapa na mtoe huduma kwa kuzingatia kanuni za Afya na usafi wa Mazingira”Alisema Mavunde

Naye Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Ndg. John Lipesi Kayombo amesema Jiji limekubali ushauri wa Mbunge kwa masharti ya wafanyabiashara hao kupangwa vizuri na kusimamia usafi wa mazingira yao.

Wakishukuru kwa pamoja,Wafanyabiashara wadogo na Mama Lishe wa Stendi Kuu Dodoma wameishukuru serikalinya awamu ya sita chini ya  Rais Dkt. Samia S. Hassan kwa kuwajali na kuwasikiliza na kumpongeza Mbunge Mavunde kwa kusimamia na kuwajali.




Share To:

Post A Comment: