Na Eleuteri Mangi, Arusha
Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA),Tumaini Nyamhokya amefunga mashindano ya Michezo ya Mei Mosi Taifa 2024 jijini Arusha kwa kuwakabidhi makombe ya ushindi wanamichezo walishinda katika michezo mbalimbali naoshiriki kwenye michezo hiyo.
Hafla hiyo imefanyika Aprili 29, 2024 katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini humo ambapo amewahimiza wafanyakazi na wananchi wote wamehimizwa kushiriki michezo ikiwemo kufanya mazoezi kuimarisha afya zao ili kukuza uchumi wao na kujiletea maendeleo wakiwa na afya bora.
Timu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imeibuka washindi wa jumla kwa kujikusanyia alama 23 katika michezo mbalimbali walioshiriki, mshindi wa pili ni Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ambayo imejikusanyia alama 16 na mshindi wa tatu ni Wizara ya Uchukuzi ambao wamejikusanyia alama 11 katika michezo yote.
Timu za Wizara mbili ambazo ni Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa zimekuwa na wakati mzuri katika Michezo ya Mei Mosi mwaka huu kwa kuwa washindi wa jumla katika mchezo wa riadha.
Katika mchezo wa riadha wanaume, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imejikusanyia alama 23 huku Wizara Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ikijukusanyia alama 15 wakati kwa upande wa wanawake Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imejikusanyia alama 20 na Wizara Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imejikusanyia alama 14.
Kwa ushindi huo, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imejikusanyia makombe tisa (9) katika michezo mbalimbali waliyoshiriki katika mashindano hayo na medali 12 walizopata katika mchezo wa riadha kwenye mbio za mita 100, 200, 400, 800, 1500 na 3000 kwa wanaume na wanawake huku Wizara Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ikijikusanyia makombe saba (7) katika michezo waliyoshiriki kwenye mashindano hayo na kujikusanyia medali 12 katika mchezo wa riadha kwenye mbio hizo.
Washindi hao wa Michezo ya Mei Mosi 2024 watakabidhiwa zawadi zao na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) ambayo yatafanyika jijini Arusha
Michizo iliyoshindaniwa ni mpira wa miguu, netiboli na wavu, kamba, riadha, baiskeli na michezo ya jadi ikijumuisha mchezo wa karata, bao, draft, darts kwa wanaume na wanawake.
Aidha, wazee wa umri wa kuanzia miaka 52 wakichuana vikali katika mchezo wa riadha kwa wanaume na wanawake katika mbio za mita 100 wa washindi kwa wanaume mshindi wa kwanza ni Juma Chikuku kutoka Wizara ya Kilimo, mshindi wa pili ni Samuel Laizer kutoka RAS Arusha na mshindi wa tatu ni Juma mbwambo kutoka WCF na kwa upande wa wanawake Judith Orunda kutoka Wizara ya Uchukuzi amekuwa mshindi wa kwanza, nafasi ya pili ikienda kwa Janeth Petro kutoka Wizara ya Maji na mshindi wa tatu ni Fatma Sif kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Michezo ya Mei Mosi 2024 imekuwa na mafanikio makubwa ikilinganishwa na miaka mingine ambapo taasisi 56 zimeshiriki kwa kuleta wanamichezo kwenye mashindano hayo kutoka mashirikisho manne ambayo ni SHIMIWI, BAMATA, SHIMISEMITA na SHIMUTA.
Post A Comment: