NA WILLIUM PAUL, MWANGA.

WAZIRI Mkuu mstaafu na Makamu wa Kwanza wa Rais, Cleopa David Msuya amewaonya viongozi wa chama cha Mapinduzi na Serikali wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro kujiepusha na migogoro isiyo ya lazima kwa maslahi mapana ya wananchi wa Mwanga.

Msuya alitoa kauli hiyo wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa ofisi ya Chama cha Mapinduzi kata ya Kigonigoni wilayani Mwanga ambapo alisema kuwa, wapo baadhi ya watu wamekuwa wakiacha kazi zao na kujiingiza katika migogoro ya kushughulikia watu kwa maslahi yao binafsi na kuwataka Viongozi kutotumika.

“Mmesikia hapa huyu kijana Rajabu Manyinya alipoanza kujitolea kwa ajili ya ujenzi wa hii ofisi ya chama kata wapo watu wanafikiri anatafuta nafasi ya kugombea wanaacha kazi zao na kuanza kumshughulikia kwani hizo nafasi walizonazo ni zao chama kimesema kila baada ya miaka mitano mwanachama wa ccm anahaki ya kuchagua na kuchaguliwa kitakachokuweka wewe milele katika nafasi yako ni jinsi utakavyotoa huduma nzuri kwa wapiga kura wako” alisema Msuya.

Na kuongeza “kawaida hawa watu wenyekupita na kueneza maneno ya uongo sio wa kufanya kazi sio watu waliojitolea kwa ajili ya wapigakura wao maana kama wangekuwa wamejitolea vizuri wasingekuwa na wasiwasi”.

Aidha Waziri Mkuu mstaafu huyo alitoa wito kwa viongozi wa CCM kuwa imara kwa kudhibiti watu wanaoeneza uongo kwa Wananchi wa wilaya ya Mwanga kwani kama anatafuta nafasi ya kuchaguliwa ndani ya chama kama Diwani, Mbunge au Mwenyekiti anapaswa kufuata utaratibu.

“Ninyi chama ndio mnaopitisha majina ya wagombea watu wenye tabia ya kueneza uongo futeni majina yao katika wilaya yetu ya Mwanga kwani mkifanya hivo hakutakuwa na tatizo lakini tunapoteza muda mwingi na gharama nyingi na fedha nyingi za kuhongahonga ili waendelee katika nafasi ya kuchaguliwa kunafaida gani” alisema Msuya.

Kiongozi huyo alisema kuwa, dawa ni chama kusimamia misngi yake ambapo wakiona watu wanapitapita na kutoa vizawadi na kujitangazatangaza kuandika majina yao na kipindi cha uchaguzi utakapofika kupendekeza majina hayo kuwa hayafai na kutoa sababu za wazi kuwa walianza kampeni mapema.

Aliongeza kuwa, Wanachama wa CCM Mwanga wataendelea na moyo wa kushirikiana na kuwa na mshikamano na umoja pamoja na kufuata mila za kipare zilizo nzuri.

Kwa upande wake, Katibu Mwenezi wa CCM mkoa wa Kilimanjaro, Ibrahim Urio alisema kuwa, mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi wa Serikali za mitaa na kuwaasa wananchi na Wanachama wa CCM kuwachagua viongozi bora wa serikali za mitaa kwani ndio injini ya maendeleo.

Urio alisema kuwa, chama kinachoweza kuwatumikia wananchi na kuwaletea maendeleo ni chama cha Mapinduzi pekee n akuwasihi kuchagua viongozi wanaotokana na chama kinachoongoza dola.

Aidha alitoa wito kwa wananchi kusimamia na kuilinda miradi inayoletwa na serikali kwa maslahi mapana yao na iweze kudumu kwa muda mrefu zaidi.

Naye Mwenyekiti wa Ujenzi wa Ofisi hiyo ya kata ya Kigonigoni, Rajabu Manyinya alisema kuwa, alipata wazo la kureja ofisi hiyo ili kurudisha shukrani kwa chama cha Mapinduzi kwa yale yote aliyofanyiwa kupitia kwa Waziri Mkuu Mstaafu, Cleopa Msuya ambapo alimsomesha sekondari hadi kuhitimu elimu yake ya juu.

Manyinya alisema kuwa, ofisi hiyo inatarajiwa kugharimu milioni 24 mpaka kukamilika kwake ambapo katika uwekaji wa jiwe hilo la Msingi Msuya aliongoza harambee na kukusanya milioni 20 za ujenzi.







Share To:

Post A Comment: