NAIBU  Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi amemuagiza Meneja wa RUWASA  Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Rebman Ganshonga,  kuhakikisha anapeleka huduma ya maji kwenye vitongoji ambavyo bado havina huduma ya maji.

Mhandisi Mahundi ametoa maagizo hayo leo Machi 17, 2024  akiwa katika muendelezo wa ziara ya kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira ya kukagua utekelezaji wa miradi ya Maji Mkoani Ruvuma 

Akiwa ziarani pia Mhandisi Mahundi ametoa rai kwa wananchi kuendelea kutunza vyanzo vya maji ili miradi ya maji iwe endelevu.

Nae Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira  Mhe.Jackson Kiswaga ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Maji kwa usimamizi na utekelezaji wa miradi. 

"Mradi huu ukamilike kwa wakati pia wananchi muweze kutunza Miundombinu yake ili mradi uwe endelevu. Lakini chombo cha watumiaji maji katika  jamii kiundwe ili kiweze kukusanya fedha na kufanya matumizi mazuri ya ukarabati wa mradi pindi  inapotokea mradi umeharibika"amesema Mhe.Kiswaga

Akitoa taarifa ya  utekelezaji wa mradi wa maji  Malungu Meneja wa RUWASA Wilaya ya Nyasa Mhandisi  Masoud Samila amesema mradi wa  Malungu unatekelezwa  kwa gharama  ya Shilingi Bilioni 1.2 

Mhandisi  Samila amesema kukamilika kwa mradi huo kunalenga kuwanufaisha wananchi wapatao 9,659 kutoka vijiji vya Malungu na Tingi vilivyopo katika kata ya Tingi.

" Mradi pia utasaidia kupunguza magonjwa mbalimbali ya mlipuko kwa jamii. Vilevile kutokana na kuimarika kwa huduma ya maji, jamii itapata muda wa kufanya shughuli za maendeleo"amesema Mhandisi Samila







Share To:

Post A Comment: