SERIKALI imeutaka uongozi wa Mamlaka ya Serikali mtandao kushirikiana na mamlaka zingine za ulinzi na usalama kutafuta suluhu ya kudhibiti matapeli wanaotumia mtandao kuibia watu jambo ambalo limekuwa likigombanisha Serikali na wananchi inayowatumikia.
Wito huo umetolewa leo Februari 8, 2024 na Naibu Waziri wa nchi ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete katika hotuba yake ya kufunga mkutano wa kikao kazi cha nne cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) uliokuwa ukifanyika jijini hapa.
Naibu Waziri Kikwete amesema matapeli wamekuwa kero kubwa kwa nchi na mbaya zaidi wamekuwa wakiwatapeli watu masikini ambao Uchumi wao ni mdogo kwa kutumia matangazo ya uongo huku wakiwadai fedha.
“Binafsi nilishawahi kutapeliwa na bwana mmoja ambaye alinipigia simu akidai kuwa tunafahamiana na alikuwa na tatizo, na mimi bila kujua nilimtumia fedha lakini baadae ndio nikaja kugundua nimetapeliwa, amesema na kuongeza:
“Hawa jamaa wanatumia akili nyingi sana, wanaweza ku edit matangazo mbalimbali na kuwatumia watu, unakuta mtu ni maskini na ana uhitaji wa huduma hiyo kama ni kazi au masomo na mwisho akitakiwa kutuma fedha atatuma na hapo anakuwa kisha tapeliwa, hii sasa ni mbaya sana, niwatake tu watendaji wa eGA, muangalie namna ya kufanya kuthibiti hili tatizo.”amesema.
Amesema Serikali itahakikisha maombi mbalimbali yaliyowasilishwa na mamlaka hiyo itayatekeleza kwa wakati ili kurahisisha utendaji kazi wa mamlaka hiyo hususani kuharakisha taasisi zote za Serikali zinaunganishwa Pamoja.
Aidha amewataka wakuu wa Taasisi za Serikali kuhakikisha wataalam wa Tehama katika taasisi zao wanaendelezwa kitaaluma ili kuendana na mabadiliko mbalimbali ya kiteknolojia ambayo imekuwa ikikua kila siku.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao Mhandisi Benedict Ndomba amesema katika kikao hicho wameweza kubainisha changamoto mbalimbali ikiwemo udurufu wa taarifa za Serikali lakini wameshaweka mikakati ya kukomesha hali hiyo.
Ndomba amesema zaidi ya wadau 3,000 wameweza kushiriki katika kikao hicho ikiwa ni ongezeko la zaidi ya wadau 2000 waliokuwa wakitarajiwa kushiriki hapo awali jambo ambalo limeleta mafanikio makubwa kwa mamlaka hiyo na kurahisisha utendaji wake wa kazi.
Washiriki katika Kikao hicho walitoka katika taasisi na mashirika mbalimbali ya umma wakiwemo; Makatibu Wakuu, Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma, Makatibu Tawala Mikoa na Wilaya, Wakuu wa Vitengo na Idara za TEHAMA, Maafisa TEHAMA Pamoja na watumiaji wengine wa TEHAMA katika taasisi hizo kwa lengo la kujadili na kutoa taarifa ya hali ya utekelezaji wa jitihada za serikali mtandao katika taasisi za umma.
Post A Comment: