Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (OWMS) imeanza kutumia Mfumo wa Mashauri wa Mahakama wa Kieletroniki ili kuongeza matumizi ya TEHAMA, uwazi, uwajibikaji, upatikanaji wa taarifa kwa haraka na imani kwa wananchi kuhusu utendaji kazi wa vyombo vinavyotoa haki kwa wananchi.

Hayo yameelezwa na Kaimu Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, ndugu Mark Mulwambo wakati akifungua mafunzo elekezi kuhusu Mfumo wa Kieletroniki wa Mashauri ya Mahakama Kuu ya Tanzania (e-CMS) na utunzaji wa nyaraka za Serikali ambapo ufunguzi huo umefanyika leo mjini Morogoro na kusema kuwa OWMS imeona ni muhimu kwa watumishi wake kupata mafunzo kuhusu Mfumo wa Mahakama wa e-CMS ili waweze kuutumia kwa pamoja na kusomana na mfumo wa usajili wa mashauri wa OWMS (CIMS) kwa lengo la kuboresha utendaji kazi, kuongeza tija na ufanisi katika usajili, matumizi na uendeshaji wa mashauri baina ya Mahakama, OWMS, wadau na wananchi.

Ameongeza kuwa Mfumo wa e-CMS umefanikisha yafuatayo ikiwemo utoaji wa taarifa kwa wahusika wa shauri kuwa shauri lao limesajiliwa na kupangiwa Jaji au Hakimu; umetoa mwanya wa kujumuisha taarifa za taasisi nyingine za Serikali ili ziweze kutumika na kusomana;utaendana na taratibu za utendaji wa Mahakama; Majaji wanaandika mwenendo wa mashauri kwenye Mfumo badala ya kuandika kwenye majalada; unapanga mashauri kwa kila Jaji badala ya Jaji mmoja kuwa na mashauri mengi au machache

Pia, Mfumo wa Mahakama wa e-CMS umefanikisha usajili wa namba ya utambuzi wa kesi ambayo haijirudii na kutumiwa na Mahakama nyingine; umesajili taarifa za mashauri ya Mahakama ya Rufaa ambapo hapo awali haikuwepo; umetambua na kuruhusu matumizi ya taarifa kutoka NIDA, BRELA, Chama cha Mawakili wa Tanganyika, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na taarifa za taasisi nyingine; umetambua na kubaini usajili wa Mawakili na Waendesha Mashtaka halali kwa kuwatambua kwa namba zao na sio vinginevyo.

Mulwambo amewapongeza Mahakama Kuu ya Tanzania kwa kujenga Mfumo wa e-CMS kwa kuwa haki itapatikana kwa wakati kwa watu wote bila kujali mahali alipo kwa kutumia TEHAMA na kwa kuzingatia kuwa OWMS ni mdau muhimu hivyo mafunzo kuhusu Mfumo wa e-CMS yanatolewa kwa washiriki 27 kutoka OWMS na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kuwawezesha watumishi kubadilishana uzoefu kwenye masuala ya usajili wa mashauri, utunzaji wa kumbukumbu za kielektroniki na namna nzuri ya kuwahudumia wateja wa ndani na nje.

Aidha, amewataka washiriki hao kuzingatia mafunzo hayo ili waweze kutumia ujuzi watakaoupata na kuyafanyia kazi kwa kuzingatia uadilifu na usiri katika utendaji kazi kwa kuwa Masjala ya Sheria ni Ofisi nyeti katika kutunza nyaraka za Serikali.

Naye Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Masjala ya Sheria wa OWMSndugu Dennice Leonard amesema kuwa Mfumo wa Mahakama wa e-CMS utawawezesha wananchi kupata taarifa na kufuatilia mwenendo wa mashauri Mahakamani kwa kupata ujumbe kwenye simu zao za mkononi na barua pepe.

Pia, Katibu Sheria wa OWMS, Bi. Victoria Kawacha ameshukuru ujenzi wa Mfumo wa Mahakama wa e-CMS kwa kuwa utarahisisha utendaji kazi na kupunguza muda wa kuandika taarifa za mashauri na nyaraka mbali mbali kwenye majalada kwa kuwa taarifa zitapatikana kwenye Mfumo huo

Share To:

Post A Comment: