NAIBU Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI Deogratius Ndejembi amemuagiza Afisa Elimu Sekondari Mkoa wa Kigoma na Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma kutoa maelezo ya maandishi kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Adolf Nduguru ya kwanini walitoa taarifa ya kukamilika kwa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Nkungwe ilihali ikiwa bado haijakamilika.

Mhe Ndejembi ametoa agizo hilo wakati wa ziara yake ya kukagua ujenzi wa shule za sekondari katika Wilaya ya Kigoma ambapo ameeleza kutoridhishwa na ujenzi wa shule hiyo huku akimtaka Mkurugenzi wa Halmashauri kumchukulia pia hatua za kinidhamu Mhandisi wa halmashauri na mhandisi anaesimamia mradi huo.

“Namuagiza Katibu Mkuu TAMISEMI, kwanza apokee maelezo ya maandishi kutoka kwa maafisa elimu hawa ya kwanini wametoa taarifa ambazo siyo sahihi. Taarifa walizozileta kwa Ofisi ya Rais-TAMISEMI ni kwamba shule hii imekamilika jambo ambalo siyo kweli.”

“Tumekagua ujenzi huu wote na tumejionea kwamba madarasa yenyewe bado hayajakamilika, milango haijafungwa, madawati hayajawekwa na hata vyol vyenyewe bado havijakamilika. Sasa kwa uzembe huu hatuwezi kukaa kimya lazima tuchukue hatua za kinidhamu kwa wote waliohusika,” amesema Mhe. Ndejembi.

Amesema Ofisi ya Rais-TAMISEMI haitomvumilia mtu yeyote atakayejarihu kurudisha nyuma jitihada za Mhe.Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye amepeleka zaidi ya Sh. Milioni 600 kwa ajili ya kumaliza changamoto ya wanafunzi kutembea umbali mrefu.

“ Mkurugenzi wa Halmashauri nikuagize pia uwachukulie hatua watumishi wote ambao wamepewa dhamana ya kusimamia ujenzi huu ikiwemo mhandisi wa mradi huu kwa kushindwa kuwajibika ipasavyo kiasi cha kuisababishia hasara serikali lakini pia kurudisha nyuma maendeleo ambayo Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amepambana kuyaleta Kigoma,” amesema Ndejembi.

Share To:

Post A Comment: