Wadau kutoka Wizara, Bodi za Kitaaluma Vyuo, Viwanda na Taasisi mbalimbali wamekutana kujadili na kupitia na kuthibitisha Viwango vya Kazi katika tasnia za kimkakati katika kuweza kufanikisha malengo ya kitaifa.

Udhibitishaji na upitiaji wa viwango vya kazi umeratibiwa kati ya NACTVET na taasisi ya Sunmaker kutoka Jamhuri ya Watu wa China ukiwa unalengo wa kuhakikisha Viwango vya Kazi hivyo vinatumika kuongoza utekelezaji wa programu mbalimbali za mafunzo na kuandaa wahitimu wanaokidhi mahitaji ya soko la ajira.

Aidha, Viwango vya Kazi vinalenga kupunguza gharama kwa taasisi za mafunzo zinazotumika katika hatua za awali za kuandaa mitaala ambazo ni pamoja na ukusanyaji wa maoni ya wadau na mahitaji toka ulimwengu wa kazi.

Akifungua warsha hiyo, leo tarehe 22 Februari 2024 mjini Morogoro Katibu Mtendaji wa NACTVET, Dkt. Adolf Rutayuga amesema Viwango vya Kazi vina umuhimu mkubwa katika kuleta ubora, ustadi na umahiri wa wafanyakazi ndani ya tasnia au taaluma za kisekta. Amebainisha kwamba Viwango vya Kazi vinafafanua ujuzi, maarifa na umahiri unaohitajika kumwezesha mtu binafsi kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, na kuchangia mafanikio ya mashirika na taasisi yaliyowaajiri ili kuchangia ukuaji na mafanikio ya viwanda na taaluma.

Dkt. Rutayuga amewaeleza washirki wa warsha kwamba shabaha ya Baraza ni kuhakikisha vinaandaliwa Viwango vya Kazi vyenye kuakisi ujuzi na maarifa yanayohitajika katika nyanja husika na vinavyokubalika katika ulimwengu wa kazi.

“Kwa sasa nchi yetu inajenga uchumi wa viwanda ambao unahitaji wafanyakazi wenye ujuzi na sifa stahiki, hivyo kama nchi hatuwezi kukwepa kuandaa wafanyakazi wenye uwezo wa kazi na ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira”, amesema Dkt. Rutayuga.

Aidha, amewataka wadau kutosita kutoa michango ya maboresho ya Viwango vya Kazi katika sekta husika na kuwahakikishia kwamba maoni yao yatazingatiwa ipasavyo ili viwango hivyo vitakapokamilika viweze kuchangia katika kuandaa wafanyakazi wenye maarifa, ujuzi na weledi wa kazi utakaowawezesha kukabiliana na changamoto zinazoikabili jamii kwa wakati husika.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Vyuo NACTVET, Dkt. Amani Makota amesema,Viwango vya Kazi vitajibu mahitaji ya soko la ajira ambapo vyuo vitaweza kuandaa mitaala yenye kukidhi mahitaji kwa kuzalisha wataalamu wenye ujuzi na maarifa ambayo viwanda vinayahitaji.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa taasisi ya Sunmaker, Bi. Zhang Yujia, ambao ndio washirika wakuu katika kuandaa Viwango vya Kazi alisema, Viwango vya Kazi vinavyoakisi mahitaji sahihi kutoka kwa tasnia husika, vitasaidia taasisi za TVET kuandaa programu kulingana na mahitaji yaliyotajwa katika viwango vya kazi.

Warsha hiyo inafanyika kwa awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza imeanza leo na kuzihusisha programu za Ujenzi, Nishati na Usafirishaji na awamu ya pili itahusisha programu za Kilimo, Mifugo na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Share To:

Post A Comment: