Na Abdallah Nassoro-MOI
Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imekubaliana na Chuo Kikuu cha Weill Cornel cha nchini Marekani kuendeleza ushirikiano ili kufanikisha adhma ya MOI kuwa kituo cha umahiri kwa upasuaji ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu barani Afrika.
Makubaliano hayo yamefikiwa leo Machi, 26, 2024 ikiwa ni miaka 15 tangu kuanzishwa kwa uhusiano huo uliofanikisha ongezeko la madaktari bingwa wa upasuaji wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu katika Taasisi ya MOI kutoka watatu hadi 13.
Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Prof. Abel Makubi ameongoza timu ya Menejimeti ilipokutana na Mkurugenzi wa Upasuaji wa Mgongo wa Chuo Kikuu cha Weill Cornel cha nchini Marekani Prof. Roger Hartl katika ukumbi wa Premier Lounge.
Prof. Makubi amekishukuru Chuo Kikuu cha Weill Cornel kwa ushirikiano uliowezesha wataalam wa MOI kwenda kujifunza mbinu mpya za upasuaji katika Chuo hicho, msaada wa vifaa tiba pamoja na uwezeshaji wa kufanyika kwa tafiti za kitaalam.
“Tunathamini ushirikiano huu ambao umekuwa na faida kubwa kwetu, wakati uhusiano huu unaanza tulikuwa na madktari watatu lakini leo tuna madaktari 13, pia wapo wauguzi waliokwenda Weill Cornel kujifunza, msaada wa vifaa tiba na tafiti, hivi vyote vimekuwa vya umuhimu kwetu katika kuijenga MOI kuwa kituo cha umahiri cha tiba za ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu” amesema Prof. Makubi
Kwa upande wake Prof. Hartl ameahidi kuendeleza ushirikiano ili kuiwezesha MOI kuwa kituo cha Umahiri cha upasuaji wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya fahamu kwa uwekeza katika mafunzo, tafiti na vifaa tiba vya kisasa.
“Tutaendelea kushirikiana kwa kuwajengea uwezo wataalam wetu wa MOI kuwa mahiri katika teknolojia mpya za matibabu, vifaa tiba vya upasuaji na tafiti za kisayansi ili MOI iwe kituo cha umahiri kwa tiba Afrika...munaweza kuwa mahiri kwa nyinyi kutoa mafunzo kwa wataalam kutoka nchi zingine barani Afrika” amesema Prof. Hartl
Awali Daktari bingwa wa upasuaji wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu Dkt. Hamisi Shabani amesema ushirikiano huo umeacha alama kwa MOI kwa kuwezesha wataalam kujifunza mbinu mpya za utoaji wa tiba pamoja na njia sahihi za kuwatunza wagonjwa waliofanyiwa upasuaji.
Post A Comment: