Serikali kupitia Wizara ya Afya imewaasa wananchi kuacha tabia ya kutumia dawa za macho kwa lengo la kutibu ugonjwa wa ‘Red Eyes’ zisizo rasmi kwa kuwa matumizi hayo yanaweza kupelekea upofu usiotibika kama ambavyo itakuwa kwa wengi wa wagonjwa waliokwisha kupata madhara kwenye kioo cha jicho kwa kutumia vitu hivyo.

Wito huo umetokewa leo Februari 8, 2024 na Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Wizara ya Afya Prof. Paschal Ruggajo alipokua anaongea na waandishi wa habari katika ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar Es Salaam.

“Ugonjwa wa ‘Red Eyes’ hauleti upofu lakini matumizi ya dawa zisizo rasmi na zinazonunuliwa kiholela yanaweza kupelekea upofu usiotibika kama ambavyo inaweza kuwapata baadhi ya wagonjwa waliopata vidonda kwenye kioo cha Jicho baada ya kutumia dawa hizo zisizo rasmi” Amesema Prof. Ruggajo.

Amesema, Baadhi ya vitu vinavyotumika ni pamoja na dawa zenye vichocheo vya ‘steroids’ ambazo wananchi wanakwenda kununua wenyewe kwenye maduka ya dawa, tangawizi, chai ya rangi illiyokolea majani, mafuta tete yaliyokuwa yakitumika wakati wa janga la Covid – 19, maji ya chumvi na maziwa ya mama, ambavyo vitu vyote hivyo sio salama na havijaelekezwa na wataalamu.

Aidha, Prof. Ruggajo amesema hadi sasa takwimu zinaonesha ongezeko la kuenea kwa ugonjwa huu ambapo jumla ya wagonjwa 12,332 wameonwa katika vituo vyetu vya tiba na wagonjwa hawa wameonwa katika Mikoa 23 ya Tanzania Bara.

“Mikoa inayoongoza kwa ugonjwa huo ni Dar es Salaam ambapo idadi ya wagonjwa imefikia 6,412, Pwani wagonjwa 4,041, Dodoma 363, Morogoro 307, Mtwara 193, Shinyanga 193, Tanga 190, Lindi 101.” Amesema Prof. Ruggajo

Amesema Mikoa mingine ni Katavi ina jumla ya wagonjwa 94, Njombe 81, Ruvuma 77, Arusha 42, Mwanza 40, Mbeya 37, Songwe 33, Rukwa 31, Kilimanjaro 31, Geita 18, Singida 17, Kigoma 13, Simiyu 9, Mara 5 pamoja na Tabora 4.

Wizara inaendelea kusisitiza jamii kuzuia kuenea kwa maambukizi haya kwa kuzingatia usafi binafsi na kanuni za Afya ikiwa ni pamoja na Usafi wa mikono na uso, Kuzuia kugusa macho yako kadri uwezavyo, Nawa mikono na maji tiririka na sabuni au na tumia vipukusi mara kwa mara, zingatia kutokushikana mikono maeneo ya sehemu za ibada, Tumia taulo au leso za karatasi kufuta tongotongo au machozi, Fika Kwenye kituo cha kutolea huduma mara upatapo dalili hizi.

Share To:

Post A Comment: