MWENYEKITI wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) na Mjumbe wa Kamati kuu (MCC), Mohammed Ally Kawaida amesema kuwa, Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hasani itaendelea kuboresha mazingira kwa Vijana ili waweze kujiajiri wenyewe na kukabiliana na changamoto ya Ajira nchini.

Kawaida ametoa kauli hiyo alipotembelea kikundi cha Vijana kinachojishughulisha na uchapishaji cha Quality Printing Press kilichopo Moshi mjini mkoani Kilimanjaro ambapo alisema kuwa, lengo la serikali ni kutengeneza mazingira rafiki kwa Vijana kujiajiri.

Alisema kuwa, katika kuhakikisha lengo hilo linatimia Serikali itaendelea kutoa mikopo kwa Vijana kama mitaji ya kuanzisha biashara mbalimbali.

“Lengo la serikali ni kumaliza tatizo la Ajira kwa Vijana ndio maana ilikuja na mradi wa Jengo kesho iliyo bora (BBT) ambapo Vijana walipatiwa elimu ya maswala ya Kilimo pamoja na kupatiwa mashamba yenye miundombinu yote ya Kilimo pamoja na mitaji” Alisema Mwenyekiti Kawaida.

Mjumbe huyo wa Kamati kuu alisema kuwa, katika kuhakikisha Vijana wanatengenezewa mazingira rafiki ya kuanzisha viwanda ili waweze kujiajiri na kwamba serikali imeendelea kuboresha swala la upatikanaji wa umeme wa uhakika.

Kawaida alitumia pia nafasi hiyo, kuwaasa Vijana kutolalamika kuhusu Ajira na badala yake watumie fursa iliyotolewa na Serikali kwa kuanzisha vikundi na kunufaika na mikopo inayotolewa ya serikali isiyo na riba.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UVCCM mkoa wa Kilimanjaro, Ivan Moshi alisema kuwa, serikali imeendelea kuboresha upatikanaji wa elimu ikiwemo ya ufundi ili kuwezesha Vijana wanaohitimu kutumia elimu wanayoipata kujiajiri.

“Serikali ya awamu ya sita imetoa fedha nyingi kuwekeza katika sekta ya elimu ili kuhakikisha Vijana wanapata elimu na kuitumia kujiajiri na kujiletea kipato na kukuza uchumi” Alisema Ivan.

Naye Mwenyekiti wa kikundi cha Quality Printing Press, Ally Mohamed alisema kuwa, kikundi hicho ni muunganiko wa Vijana sita wakiwa na lengo la kukuza mtaji na kufanya kazi kwa pamoja ili kujikwamua kiuchumi.

Mohamed alisema kuwa, kikundi hicho kimenufaika na mkopo wa halmashauri ambapo walipatiwa milioni 18 kama mtaji ambapo kwa sasa kikundi hicho kinamtaji wa milioni 120.

Alisema kuwa, changamoto wanazokumbana nazo ni pamoja na taasisi mbalimbali kuchelewesha malipo baada ya kukabidhiwa kazi tofauti na makubaliano ya mkataba wa ununuzi.

“Tunakabiliwa na ufinyu wa eneo la kazi kutokana na kukosa kibali cha kuendeleza ujenzi eneo la nyuma pamoja na ongezeko la kodi la pango mara kwa mara kutoka kwa wamiliki wa nyumba pamoja na kodi za serikali kila mwaka” Alisema Mohamed.

Share To:

Post A Comment: