Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kimeungana na taasisi za elimu juu na taasisi nyingine nufaika za Mradi wa elimu ya juu kwa mageuzi ya kiuchumi (HEET) katika kikao kazi cha kujadili maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo kinachofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 27-29 Februari 2024.
Akifungua kikao hicho Mkurugenzi wa Elimu ya Juu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Peter Msofe amesema katika kikao hicho taasisi zitawasilisha taarifa za utekelezaji wa viashiria vya matokeo ya utekelezaji wa mradi (result indicators).
Prof. Msofe amebainisha maeneo hayo kuwa ni Maendeleo ya majenzi, kuwajengea uwezo wataalam na viongozi katika taasisi za elimu ya juu, uhuishaji na uboreshaji wa mitaala katika programu za kipaumbele, uundwaji wa kamati za ushauri za kitasnia, makubaliano yaliyoingiwa kati ya taasisi na sekta binafsi na matumizi ya TEHAMA.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi wa HEET -IAA katika kikao hicho Mratibu wa Mradi-IAA Dkt. Henry Mung’ong’o amesema IAA inatarajia kuhuisha mitaala tisa (09) ifikapo Juni 2024; ili kuendana na mahitaji ya soko, na kuanzisha mitaala mipya 10 katika Kampasi ya Babati na Kampasi tarajiwa ya Songea ifikapo Desemba 2024.
Aidha, Dkt. Mung’ong’o amesema IAA imeingia makubaliano na taasisi binafsi 23 ambazo zitasaidia kutoa ushauri wa kitaalam kwenye maboresho ya mitaala kulingana na soko la sasa, kutoa fursa kwa wanafunzi kwenda kujifunza kwa vitendo na walimu kuongeza maarifa na ujuzi kwa vitendo kwenye taasisi hizo.
Akizungumzia dhamira ya IAA katika kuboresha matumizi ya TEHAMA kupitia mradi wa HEET, Dkt. Mung’ong’o amesema IAA imeanza kufanya maboresho katika miundombinu ya maktaba ya Chuo ili kuhakikisa kuwa inatoa huduma kidijitali.
Kuhusu ujenzi wa hosteli, majengo ya kitaaluma na utawala katika Kampasi za Arusha Babati na Kampasi tarajiwa ya Songea Dkt. Mung’ong’o amesema Chuo kimeshafanya tathmini ya athari za mazingira katika maeneo husika na kinaendelea na hatua nyingine kwa ajili ya kuanza ujenzi.
Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kupitia mradi wa HEET kimepewa jumla ya Dola za Kimarekani 19,007,648 sawa na shilingi 48,469,498,473 kwa ajili ya kutekeleza vipaumbele vya mradi huo kwa miaka mitano kuanzia 2021/2022 mpaka Julai 2026.
Post A Comment: