Wanafunzi wa Stashahada ya Usimamizi wa Biashara na Lugha ya Kichina (Business Management with Chinese) katika Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) wamesema kozi hiyo ina uwanja mpana wa fursa za ajira kutokana na ukuaji wa lugha hiyo katika ulimwengu wa biashara Kimataifa.

Wanafunzi hao wamebainisha hayo leo tarehe 22 Februari 2024 katika hafla ya maadhimisho ya mwaka mpya wa Kichina yaliyofanyika katika Kampasi ya Arusha.

“Najivunia kusoma kozi hii na itanisaidia kwa sababu Kichina kina fursa nyingi maofisini, benki, kwenye makampuni na maeneo mengine; mfano sasa hivi ofisi nyingi zinafungua madawati maalum ya Kichina na watu wanaoijua hii lugha ni wachache mtu akimaliza hawezi kukaa bila kazi,” alisema Jackline Swai mwanafunzi IAA.

Naye Yusuph Mboya (mwanafunzi) amesema pamoja na fursa za ajira katika makampuni na mashirikai, kozi hii ina faida kwa walio tayari kujiajiri kwenye biashara kwa kuwa Kichina kitawasaidia katika mawasiliano ya kibiashara Kimataifa.

Kwa upande wake Meneja wa Kampasi ya Arusha (IAA), Dkt. Grace Idinga amesema kozi hii inawaandaa wataalam wa kipekee katika soko la ajira ambao wanaweza kufanya kazi kama mameneja, wahasibu na wakalimani wa lugha katika kampuni za Kichina, viwanda na sekta ya utalii.

Aidha, Dkt. Idinga amesema kuwa jumla ya wanafunzi 403 wamesoma kozi hiyo tangu ilipoanzishwa mwaka 2021 na kati yao 166 wamehitimu, huku akibainisha kuwa wanafunzi wanaoendelea na masomo kwa sasa ni 237.

Dkt. Idinga ameongea kuwa IAA inaendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi wa kozi hii, ikiwemo kuongeza walimu wa lugha ya kichina, vitabu na vifaa vingine saidizi vya kufundishia lugha ya Kichina.

Mwakilishi wa Wanajumuiya ya Watu wa China Mkoani Arusha, Bw. Feng Xian Suang amepongeza IAA kuandaa hafla hiyo ya maadhimisho ya mwaka mpya wa Kichina, ambalo amesema ni tukio muhimu kwa Uhusiano wa Kidiplomasia kati ya Tanzania na China ambao umekuwepo kwa zaidi ya miaka 60 sasa.

IAA imeadhimisha tukio hili kwa mara ya kwanza likihusisha wanafunzi wa IAA, baadhi ya wanafunzi wa baadhi ya shule za sekondari Arusha wanaosoma Lugha ya Kichina.

Share To:

Post A Comment: