Serikali kupitia Wakala wa Baraba Nchini (TANROADS), inaendelea na Ujenzi na ukarabati wa Barabara zinazounganisha Tanzania na nchi zote jirani ikiwemo nchi ya Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa, Bungeni jijini Dodoma leo Februari 7, 2024 wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Felista Njau aliyeuliza Je, kuna mkakati gani wa kuboresha miundombinu katika mipaka ya nchi yetu na nchi jirani zenye fursa za kibiashara kama DRC-Congo ili kukuza Diplomasia ya Uchumi.
1000567311
Waziri Bashungwa amesema Serikali imekamilisha ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Sumbawanga Matai hadi Bandari ya Kasanga (km 107) mkoani Rukwa na tayari Serikali imesaini Mkataba wa kujenga kwa kiwango cha lami wa barabara ya Kigwira Karema (km 112) kwenda Bandari ya Karema mkoani Katavi.
Amesema Serikali inatekeleza mpango wa kuboresha barabara ya kuanzia Igawa Mbeya – Tunduru kuwa njia nne. Pia Serikali inaendelea kuboresha Viwanja vya Ndege vya Songwe, Sumbawanga na Kigoma ambavyo vipo mpakani na DR Congo.
Aidha, Mbunge wa Kwimba, Shanif Jamal alitaka kujua Je, lini Serikali itaanza mchakato wa kutangaza barabara ya Mabuki – Jojiro hadi Ngudu ili ijengwe kwa kiwango cha lami.
Akijibu Swali hilo, Bashungwa amesema Serikali imeanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Mabuki – Jojiro – Ngudu (km 28) kwa kiwango cha lami kwa awamu ambapo mkataba wa ujenzi wa kilometa 3 kuanzia eneo la Ngudu mjini kuelekea Jojiro umesainiwa tarehe 19 Januari, 2024.
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuendelea na ujenzi kwa kiwango cha lami kwa awamu kwa sehemu iliyobaki.
Share To:

Post A Comment: