Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amewaasa Watoto wakike waliomaliza Kidato cha Nne nchini kutoruhusu mtu yeyote kuzima ndoto zao za mafakinio, badala yake wajiamini katika uwezo na nguvu za ndoto hizo katika kujiletea maendeleo na Taifa kwa ujumla.

Mhe. Kapinga amesema hayo wakati wa Mahafali ya 40 ya kuhitimu kwa Wanafunzi wa Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Kifungilo iliyoko wilayani Lushoto mkoani Tanga, tarehe 5 Desemba, 2023.

Ameeleza, Wasichana hao wamepitia changamoto nyingi hadi kufika hapo walipo sasa, lakini kutokana na bidii, uvumilivu na uamuzi usiotikisika wameweza kutoka na nguvu, hekima na uwezo wa kukabiliana na changamoto zilizopo kwenye jamii kuliko hapo awali.

Aidha, amewaasa Wasichana hao kuwa Dunia imejaa fursa zinazosubiri kunyakuliwa, hivyo uwanja ni wao katika kutumia fursa hizo ili kujiletea mafanikio na maendeleo katika maisha yao na kamwe wasiruhusu chochote kiwarudishe nyuma katika harakati za kufuata ili kutimiza ndoto zao.

" Wasichana mnapotembea Ulimwenguni mkumbuke kuwa ninyi ni Mwili wa Tumaini, Wajumbe wa mabadiliko na Viongozi bora wa baadaye wa nchi yenu, tembeeni kwa ujasiri na kwa dhamira isiyotikisika, Dunia inasubiri vipaji, ubunifu na umahiri wenu katika kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii, ninaamini uwezo huo mnao na hautakuwa na kikomo, mjiamjni", amesisitiza Mhe. Kapinga.

Vilevile amewaeleza, safari ya mafanikio ina vikwazo vingi ikiwemo kuanguka, hofu na mashaka lakini wafahamu kuwa hivyo vyote sio ishara ya udhaifu bali ni hatua na ngazi za kuelekea katika mafanikio ya kweli na kwamba kila kikwazo watakachoshinda kitasafisha dhamira zao, kuimarisha tabia zao na kuwaweka karibu na malengo yao.

Hata hivyo amewataka wasichana hao kuzungumza na watu wenye nia na malengo kama yao ambao watawahimiza, kuwatia moyo na kuwawezesha kuwa bora zaidi katika ndoto zao kwa kuwa hawako peke yao katika safari hiyo, kuna mtandao mkubwa wa usaidizi na jumuiya ya watu wanaoamini katika uwezo.
Share To:

Post A Comment: