Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema Serikali inatambua haki ya kila mtu kupata elimu na hivyo inawekeza katika kuweka mifumo na miundombinu stahiki ya kielimu Kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum nchini.

Prof. Mkenda ametoa kauli hiyo Novemba 25, 2023 mkoani Tabora akihutubia katika Mahafali ya Tisa ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Mkuu Mihayo (AMUCTA), ambapo amesema ushirikishwaji katika elimu watu wote si jambo hiari bali ni haki ya msingi ya binadamu, na ni lazima kuhakikisha kila mtu  bila kujali maumbile yake anapata elimu bora.

"Katika kutekeleza azma hii Serikali imegawa vifaa saidizi vya ikiwemo vya  kidigitali Kwa wanafunzi wenye mahitaji Maalum kuanzia Elimu ya awali, Msingi na Sekondari  vinavyogharimu zaidi ya  bilioni 3.5 na pia vifaa vya shilingi bilioni 1 Kwa ajili ya Wanafunzi wa Vyuo Vikuu" alisema Prof. Mkenda.

Ameongeza kuwa Kwa mwaka wa fedha 2023\/24 Serikali ilizindua Mwongozo wa Kitaifa wa ubainishaji na Upimaji wa wanafunzi wenye mahitaji Maalum ili kutambua mahitaji na kuweka mipango sahihi.

Waziri Mkenda amewataka wahitimu wa Chuo hicho kutambua thamani ya Elimu, na kujiandaa kikamilifu kuwajibika katika jamii kwa kuzingatia maadili utamafuni wa mtanzania na uzalendo.

Akimwakilisha Mkuu wa mkoa huo, Mkuu wilaya ya Tabora Mhe. Lous Bura ameupongeza Uongozi wa chuo hicho Kwa kazi kubwa inalenga kuchangia utoaji elimu Jumuishi nchini na ameahidi kuendelea kushirikiana katika kuendeleza elimu katika Mkoa wa Tabora na jamii kwa ujumla.

Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Mihayo (AMUCTA) Pd. Prof. Juvenalis AsanteMungu ameishukuru Serikali kuendelea kuimarisha miundombinu ya Elimu ikiwemo kwa watu wenye mahitaji Maalum na kwa kuhakikisha Toleo jipya la Sera linatambua umuhimu wa Elimu Jumuishi .

Prof. AsanteMungu pia ameishukuru Serikali kuendelea kushirikiana na chuo hicho kwa kutoa eneo la Ifucha kwa ajili ya kujenga majengo ya Kudumu ya chuo.

Wanachuo 359 wamehitimu na kupata Shahada ya kwanza ya Sanaa na Elimu, Shahada ya kwanza ya usimamizi wa biashara na shahada ya kwanza ya Elimu Maalum.
Share To:

Post A Comment: